Kihongosi akemea michango shuleni

MUSOMA: Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi ameelekeza suala la michango mashuleni likome, na kuhakikisha wananchi wanatendewa haki kwa kupata huduma kwa mujibu na maelekezo ya serikali ili kuepuka kutengeneza mazingira ya kuonekana wanaweka vikwazo kwa wananchi wao.
Kihongozi ameeleza hayo Mei 14,2026 alipokuwa akizungumza na kusikiliza kero za wananchi katika viwanja vya Mkendo Musoma Mjini mkoani Mara, ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kikazi katika mkoa huo.

Kihongosi ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea changamoto ya mama mmoja ambaye hakujitambulisha kwa majina yake alidai kuwa na changamoto ya uwezo na kushindwa kusomesha watoto wake akieleza kuwa moja ya watoto hao yupo kidato cha nne lakini ameshindwa kwenda shule kwa sababu hana uwezo wa kumlipia fedha ya kambi ambayo ni zaidi ya Sh 600,000.
Baada ya kusikia Changamoto hiyo Kihongosi alimuita Ofisa Elimu Sekondari wa Mkoa wa Mara, Aviti Malya ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo alidai kuwa ni kweli kuna utaratibu huo lakini ni kwa wazazi wenye uwezo na kiasi kinachotakiwa kulipwa ni Sh 680,000 kwa ajili ya kulipia umeme, maji na mahitaji mengine muhimu wawapo kambini hapo.

Baada ya kusikilia hilo Kihongosi alisema suala hilo bado ni changamoto na linaleta ukakasi kwa sababu kama ni watoto wa darasa moja na ni masomo sawa, hakukuwa na ulazima wa kufanya hivyo na badala yake wangewaambia wazazi wachangie chakula ili kuwasaidia watoto hao kuliko kutoa kiasi hicho cha fedha.
“Kwanini hamkwenda na utaratibu wa kuchangia chakula na sio fedha labda
Mpeleke mahindi au maharage au mchele, wa sababu la Sh 600,000 haina tofauti na shuke binafsi na kama serikali tunahubiri kwamba tunatoa elimu bila malipo sasa hoja kama hii sioni uhalali wake mimi binafsi,” amesema Kihongosi.

Ameongeza; “Tuchukue kama halmashauri sasa kwa maana nyepesi ni kwamba mnaichonganisha serikali na wananchi, hiyo ndiyo lugha nyepesi, mimi naheshimu watumishi wa umma kwa sababu mimi nimekuwa mtumishi wa umma lakini kwenye jambo kama hili kuna watu mutatafuta lawama ionekane hawa watendewi haki Kitu ambacho sio kizuri”.
Baada ya kuzungumza hayo Kihongosi aliahidi kytoa kiasi cha Sh 600,000 kwa mama huyo ili akamlopie mtoto wake, huku akiwataka watumishi kutafakari kama wanatii maagizo ya serikali au wanafanya mambo tofauti na maagizo ya serikali na chama kinasema elimu bila malipo toka kidato cha kwanza mpaka kidato cha sita.



