DK Bashiru Ally Kakurwa anajua anachokisema? Hili ni swali tunaloweza kujiuliza baada ya Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kusimama hadharani na kuanza kuirushia madongo serikali ya chama chake.
Bashiru alitumia mwavuli wa Mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) uliofanyika mkoani Morogoro kupeleka chuki zake kwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake.
Utumishi wa Bashiru ndani ya CCM ulikoma alipopelekwa Ikulu kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli. Baada ya kifo cha Magufuli, aliondolewa Ikulu na kutunukiwa ubunge wa kuteuliwa. Hapa ndipo mambo yalipoanzia.
Alionesha chuki na hasira za wazi. Kama hiyo haitoshi, akadaiwa kuwa mmoja wa watu wanaoongoza mtandao wa ‘Sukuma Gang’ kama njia ya kuisulubu serikali ya Rais Samia.
Bahati mtandao huo haukuwa na nguvu na ukagonga mwamba.
Wapo wanaoeleza kuwa, hata ubunge wake ni hisani tu juu yake maana wapo waliostahili zaidi yake katika kundi la wanachama na makada wengi wa CCM.
Ni hisani hiyo hiyo aliyopewa kutokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenda kuwa Katibu Mkuu wa CCM, baadaye Katibu Mkuu Kiongozi.
Wengi wanajua ujio wa Bashiru CCM haukupokelewa vizuri na wapenzi na wanachama wa chama hicho kikongwe nchini. Inafahamika na wengi kuwa alipokuwa UDSM anafundisha, alijikita katika mlengo wa siasa za upinzani, hasa Chama cha Wananchi (CUF).
Wachache waliunga mkono uwapo wake wakidhani misimamo yake itajenga mfumo mzuri na hadhi ya CCM mbele ya macho ya wale waliodhani chama chao kimepoteza mvuto.
Ikawa tofauti na wengi walivyodhani, alipokuwa na madaraka ndani ya chama wale waliokwenda kinyume na kile walichokitaka, walishughulikiwa vilivyo.
Ndio maana najiuliza, Dk Bashiru anajua anachokisema na kukiamini? Nina hofu hajui chochote. Na kama anakijua, basi atakuwa amejisahau kuwa kinachofanywa wakati huu ni mwendelezo tu wa kile walichokianzisha wao.
Hayo na mengine mengi yanamuanika msomi huyu. Anajitukanisha na kujivua nguo mchana kweupe. Dk Bashiru anashindwa kuchutama hali ya kuwa nguo zake zimevuka. Msomi huyu aliyewahi kujipatia sifa wakati anafundisha chuo kikuu sasa ameamua kutembea bila kujua kaptura aliyovaa imechanika, hastahili kupita nayo mitaani.
Nafasi yake ilisababisha watu kufukuzwa ndani ya chama na wengine chini ya uongozi wake walipata misukosuko ya kisiasa baada ya kuitwa kwenye vikao vya chama kujieleza.
Baadhi waliopata msukosuko ni mzee Yusuph Makamba, Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana, Nape Nnauye na January Makamba. Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Benard Membe alifukuzwa.
Waandishi wa habari (baadhi) na vyombo vyao waliamuriwa kuandika vile tu vinavyomfurahisha Bashiru na watu wake, wakiamini wanachokifanya kilimfurahisha rais aliyekuwa madarakani.
Inashangaza leo Dk Bashiru anachukizwa na watu wanaojaribu kusifia utawala wa Rais Samia. Kama ni roho mbaya, chuki, unafiki na uzandiki wa kisiasa, kwake ni wa hatari.
Kwamba anachukizwa na neno ‘mama anaupiga mwingi’? Wanasahau ni wao waliomuita Magufuli majina ya sifa, wakaenda mbali na kumfananisha na mitume ili tu wamsifie na kumfurahisha? Ni wakati huo ambao vikundi vya kutukana viongozi viliota kama uyoga.
Bashiru na wenzake hawakuona hata yale malalamiko ya wastaafu waliohoji uwapo wa watu wanaowadhalilisha. Msemo wa wastaafu wanawashwawashwa ukaibuka na kuongeza wigo wa matusi hata kwa watu wasiojua chochote kuhusu chama na uongozi wao.
Bashiru alikuwa wapi wakati huo? Nadhani angesimama nyakati zile akilalamika watu kusifia bila sababu, ningeamini ni mwerevu na mwenye nia njema kwa taifa letu. Si kama anavyofanya sasa. Nionavyo Bashiru analilia ukatibu mkuu wake. Ama anajaribu kufanya vitu vyenye baraka na mtandao wa ‘Sukuma gang’.
Dk Bashiru akikerwa na wanaosifia serikali ya Rais Samia, ajue hao hawafanyi makosa. Ni kama ilivyokuwa kwao tu.
Ajue pia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia ni rafiki mkubwa wa wakulima. Wakulima ni waelewa. Wanajua kila kinachofanyika juu yao. Ni kipindi cha uongozi wao ambacho bei ya mbolea ilipanda bei. Ongezeko lile lilisababisha Rais Samia kutoa ruzuku ya Sh bilioni 150 ili kupunguza bei ya mbolea kama njia ya kuondoa mkwamo kwenye sekta ya kilimo.
Hata kwenye eneo la tafiti za kilimo, serikali imeongeza bajeti kutoka Sh bilioni 7.3 kwa mwaka 2020/21 hadi Sh bilioni 40 kwa mwaka huu wa fedha. Pia serikali imeanzisha utaratibu mzuri wa kuwawezesha wakulima nchini kupata mbegu za alizeti. Gharama zote kwa sasa ni Sh 3,500 tofauti na bei ya zamani ya Sh 7,000 hadi 8,000. Wakulima wanajua kuhusu hili.
Serikali ya Awamu ya Sita imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo. Imeongeza bajeti ya uzalishaji wa mbegu kutoka Sh bilioni 10.5 hadi Sh bilioni 43.03.
Kama hiyo haitoshi, amewezesha kupatikana kwa bajeti bora ya kilimo ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 Wizara ya Kilimo imetengewa Sh bilioni 751, huku bilioni 631 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Bashiru anapaswa kufahamu kuwa ongezeko la bajeti ya kilimo kwa mwaka huu ni kubwa kwa asilimia 300. Kwa mwaka 2020/21 kiasi cha Sh bilioni 229 kilitengwa na kati ya fedha hizo Sh bilioni 150 ndio zilienda kwenye maendeleo.
Kama yeye hayajui haya, anataka wengine wachukie kwa kufuata chuki zake binafsi? Hii haiwezekani. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.
Bashiru wakati wake alijua namna serikali ilivyokopa fedha nyingi kuliko wakati wote wa marais wa nchi hii. Hawajasema chochote. Badala yake walisimama hadharani na kusifia kadiri walivyoweza. Huu ulikuwa unafiki wa kiwango cha juu kwa wasomi kama Bashiru.
Ni wazi Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliingia madarakani na kurithi madeni mengi aliyopambana nayo na kufanikiwa kuingiza nchi katika Mpango wa Kusamehe Madeni kwa Nchi Maskini (HIPC). Hadi Mkapa anatoka madarakani, Tanzania ilibakiza deni la Sh trilioni 20 tu.
Deni hilo liliongezeka wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Dk Jakaya Kikwete na kufikia Sh trilioni 23. Wakati anatoka madarakani, deni lilifikia Sh trilioni 43. Kwa kipindi cha miaka mitano cha Dk Magufuli, deni la taifa likaongezeka kwa Sh trilioni 29 na kufikia Sh trilioni 72.
Haukuwa mwendo mzuri wa ukopaji wa nchi masikini kama Tanzania. Lakini wanaojitia wajuaji hawakusema hili kwa minajiri ya kuelekeza serikali badala yake tuliwaona wakisimama hadharani kusifia.
Inakuwaje leo? Sote ni mashahidi. Nchi imetulia na inaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Heshima na amani imeshika kasi. Wananchi wanaishi kwa kushirikiana, kusaidia na kuthaminiana.
Mipaka ya nchi imefunguka, wageni wanaingia kwa wingi na kuongeza pato la taifa kwa kupitia sekta ya utalii. Nchi imeweka utaratibu mzuri katika sekta ya afya kwa kuruhusu watu kuchanjwa ili kujikinga na magonjwa hatari kama corona.
Rais Samia ameiweka nchi katika misingi ya ukweli na uwazi. Watanzania wote tumeshuhudia Rais Samia akitangaza nchi yetu kupokea mkopo wa kujikinga na madhara ya Covid-19 wa Sh trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF). Kama hiyo haitoshi, serikali ikaweka mchanganuo wa namna fedha hizo zinavyotumika.
Rais Samia ameamua kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa na Magufuli ili ikamilike kwa wakati huku akianzisha na miradi mingine.
Huyu ndiye Rais Samia ambaye licha ya kujishusha na kuongoza nchi kwa busara, hekima na unyenyekevu, bado wanafiki kama Bashiru hawamuelewi na kuendeleza nongwa zao.
Ndio maana nasema Dk Bashiru anajiharibia sifa yake. Kinachoendelea kumtokea ni kuzidi kumuumbua kwa sababu anajulikana mwanzo na mwisho wake kisiasa.
Kama hana la kusema anyamaze Rais Samia awatumikie Watanzania wenye mapenzi mema na taifa lao.
Mwandishi wa makala haya ni mwandishi kitaaluma na mchangiaji wa gazeti hili.