WAZIRI wa Madini, Dk Doto Biteko ametaka uongozi wa Kampuni ya Williamson Diamond LTD inayochimba madini ya almasi iliyopo Mwadui wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kuanza kazi ya uzalishaji wa madini hayo Julai 15, mwaka huu.
Kauli hiyo imekuja baada ya kampuni hiyo kusitisha uzalishaji takribani miezi sita tangu bwawa la maji tope libomoke na tope kusambaa kwenye kaya na mashamba ya watu.
Dk Biteko aliyasema hayo jana baada ya kufanya ziara ya kutembelea bwawa la maji tope jipya lililochimbwa kuanzia mwezi Machi likiwa na ukubwa wa hekta 57.2 na litakalo dumu kwa muda wa miaka miwili na nusu.
Alisema uzalishaji wa almasi uanze tarehe hiyo na kibali watapewa wiki ijayo siku ya Jumanne kwenye ofisi ya Mhandisi Mkuu wa Tume ya madini na kibali cha watu wa bonde la maji kitashughulikiwa na kuwa hawana sababu ya kushindwa.
“Nina upongeza uongozi wa mgodi huu, serikali ya mkoa na wilaya kwa ushirikiano mzuri mlio uonyesha kwani mlisimama hakuna siasa iliyoingizwa na kila mwananchi aliyeathirika kapata haki yake,” alisema.
Mkaguzi Mkuu kutoka Tume ya Madini, Henry Nditi alimueleza Biteko kibali kipo muda wowote watakapohitaji kwani bwawa hilo limeonekana kukamilika kiasi kikubwa.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Modest Mkude alisema hakuna mgogoro wowote katika eneo hilo na kwamba hali ni shwari na asilimia 96 ya wanachi walioathirika wamelipwa fidia.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Boniface Butondo alisema anaishukuru serikali kwa kuchukua hatua na kulisimamia suala hilo ambalo limeenda vizuri kwani mgodi huo umesaidia kunyanyua uchumi wananchi wa wilaya hii kwa kulipa mapato na kutoa ajira.
Meneja Mkuu wa mgodi wa almasi Mwadui, Ayoub Mwenda alisema wao wako tayari kuanza uzalishaji kuanzia wiki ijayo wanachosubiri ni kibali kutoka ofisi za madini kwani bwawa hilo limekamilika na mitambo iko vizuri.
Mhandisi kutoka kampuni ya City Engineering Anael Macha ambaye alikuwa akichimba bwawa hilo alisema lilianza kutengenezwa mwezi Machi, mwaka huu na sasa limekamilika na litadumu kwa muda wa miaka miwili na nusu na lina ukubwa wa hekta 57.2