Dk Biteko ataka kasi usambazaji umeme vijijini

KAGERA: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa REA 3 mzunguko wa pili kuongeza kasi ya kuunganisha umeme katika vijiji vyote mkoani Kagera vilivyoko katika mkataba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Ametoa kauli hiyo wakati akiwasha umeme katika vijiji vya Ntanga na Kaburanzwili Wilaya ya Ngara, ambapo alisema kuwa katika awamu hiyo ya utekelezaji wa mradi wa REA mkoa wa Kagera umefikia asilimia 77 ya utekelezaji na hakuna kijiji kitakachobaki kila kijiji kitapata umeme.

Amesema baada ya serikali kumaliza utekelezaji wa miradi ya umeme katika vijiji, mradi wa usambazaji wa umeme katika vitongoji itaanza mara moja, hivyo amewataka wananchi kuhakikisha wanafanya kazi za kuinua uchumi wao kupitia umeme, ili kujiongezea kipato.

“Umeme ni uchumi, naamini kupitia umeme huu wananchi mtanufaika vya kutosha katika kuhakikisha mnaanzisha biashara zenu, mkaingize kipato katika familia zenu, lakini pia nimuombe mkandarasi kuongeza kasi ya kusambaza umeme katika vijiji vyote kwa sababu serikali haina changamoto ya fedha, fedha ipo.

“Jambo lingine sipendi kuona vibarua wanalalamika naomba walipwe mara moja fedha zao ili wafanye kazi bila wasiwasi, “amesema Biteko.

Mbunge wa Jimbo la Ngara, Ndaisaba Ruhoro amesema uwepo wa umeme utakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wananchi, huku akisema kwa muda mfupi ambao umeme umeanza kuwaka vijijini tayari shughuli za kiuchumi zimeongezeka.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button