KILOMBERO, Morogoro: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amelitaka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha linatafuta suluhisho la kufeli kwa mfumo wa Gridi ya Taifa mara kwa mara, kwa kufanya upembuzi wa kina ili kuboresha miundombinu kwenye gridi hiyo.
Dk Biteko amesema hayo leo alipofanya ziara ya dharura katika mitambo ya kufua umeme ya Kidatu, mkoani Morogoro kufuatia kufeli kwa mfumo wa Gridi ya Taifa jana usiku na kusababisha mikoa mingi Tanzania Bara na Zanzibar kukosa umeme.
“Nawaomba radhi sana wananchi na watanzania kwa ujumla kufuatia hitilafu hiyo kwenye mfumo wa gridi, kwani imeleta usumbufu na changamoto kwa wananchi kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi kusimama,” amesema Biteko
Amesema matatizo kama hayo yanapojitokeza yawe funzo yasijitokeze tena, hata hivyo hakusita kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na timu yote ya wataalamu kwa kuchukua hatua za haraka kufika kwenye eneo la changamoto bila kusukumwa bali kwa kujiongeza.
Pia, amewatahadharisha TANESCO kuchukua tahadhari hususan katika kipindi hiki cha kiwango kikubwa cha mvua zinazonyesha na kuwataka kuchukua tahadhari kwani kiwango cha maji yanayoingia kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ni kikubwa na kutolea mfano wa kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere ili kuondoa madhara yanayoweza kusababishwa na wingi wa maji hayo.