WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana ameielekeza menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kubuni mikakati ya kuongeza mapato yatokanayo na utalii ikiwa ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Chana ametoa kauli hiyo leo Oktoba 16, alipozungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika ofisi zao zilizopo jijini Arusha.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya lakini Mheshimiwa Rais anataka tuongeze mapato na tubuni mazao mapya ya utalii,” amesisitiza.
Waziri Dk Chana ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kutoa ufumbuzi wa changamoto ya magugu vamizi yanayoharibu uoto wa asili ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
SOMA: FITI watakiwa kutangaza bidhaa za misitu
“Natoa siku saba kwa TAFORI waende katika Bonde la Kreta na kutoa ufumbuzi wa namna ya kudhibiti mimea vamizi,” amesisitiza Dk Chana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameielekeza menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kubuni mikakati ya kuongeza mapato yatokanayo na Utalii ikiwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. pic.twitter.com/NEbaXljwIR
— Wizara ya Maliasili na Utalii (@MNRT_Tanzania) October 16, 2024
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia utalii, Nkoba Mabula ameitaka mamlaka hiyo kuwa wabunifu, kuangalia namna ya kujitangaza na kubuni mazao mengine ya utalii ili kuiongezea serikali mapato.
Kikao hicho ni muendelezo wa vikao kazi vya Waziri wa Maliasili na Utalii kusikiliza changamoto za Watumishi na kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi.