Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana katika kulinda rasilimali za maliasili za nchi hizo kwa manufaa ya kizazi cha kilichopo na baadaye.
Dk Chana amesema hayo katika Mkutano wa 10 wa Baraza la Kisekta la Usimamizi wa Mazingira na Maliasili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika leo Novemba 1,2024 jijini Arusha.
“Masuala ya kimazingira yanayotukabili ni kama vile uharibifu wa misitu, uhaba wa maji, upotevu wa bioanuwai na athari za mabadiliko ya tabianchi hivyo ni budi tufanye kazi kwa ushirikiano ili kulinda na kusimamia rasilimali hizo,” amesema Chana.
Awali akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva alisema kuwa majadiliano ya mkutano huo yalijikita katika kukuza ushirikiano na kuimarisha mifumo ya kusimamia na kulinda maliasili zilizopo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Uundwaji wa Mkakati na Mpango Kazi wa Kanda ya EAC wa Bioanuwai 2025-2034 ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kulinda maliasili zetu za mazingira, pia ninaamini kuwa Mkakati na Utekelezaji wa Uchumi wa Bluu wa Afrika Mashariki utasaidia katika kuhimiza juhudi zetu za kutumia rasilimali nyingi za bluu katika eneo hili kwa ajili ya ustawi wa wananchi wetu” alisisitiza Nduva.
Alifafanua kuwa wakati majadiliano ya mkutano huo yanaendelea eneo la Afrika Mashariki limejaliwa kuwa na aina mbalimbali za mifumo tajiri ya ikolojia inayodumisha maisha ya jamii, rasilimali muhimu na kusaidia uchumi huku akiweka bayana kuwa changamoto kubwa zinazotishia utajiri huo ni kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, matumizi ya ardhi yasiyo endelevu, na upotevu wa viumbe hai yanahitaji uangalizi wa haraka.
Lengo la mkutano huo pamoja na mambo mengine ni kupitia na kujadili taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio na maelekezo ya Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Mazingira na Usimamizi wa Maliasili na Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki.