MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango, amezindua Jengo la wodi ya wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza leo na kuwaasa wavuvi wa mkoa huo na kanda ya ziwa kwa ujumla kuacha kutumia dawa zisizofaa katika uhifadhi wa samaki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mpango amesema namna bora ya kudhibiti ongezeko la wagonjwa wa saratani katika mkoa huo ni kuacha kutumia dawa hizo zisizofaa.
Akisisitiza juu ya hatari ya matumizi ya dawa hizo, alinukuu na kusema takwimu zinaonesha ugonjwa wa saratani bado ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza duniani kwa kusababisha vifo kwa watu wengi, ambapo Tanzania takribani watu 42,000 kila mwaka hupata ugonjwa huo.
Aliziagiza mamlaka za udhibiti kuhakikisha zinakomesha jambo hilo mara moja, huku akisema kuwa serikali inawekeza katika ujenzi wa miundombinu, ili kuhakikisha huduma za matibabu ya saratani zinasogezwa karibu na wananchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanzisha kiwanda cha mionzi dawa, kitakachosaidia utoaji huduma kwa wagonjwa wa saratani.