Dk Mpango ataka huduma za kibenki vijijini

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amezitaka benki nchini kupeleka huduma zao maeneo ya vijijini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki vijijini.

Dk Mpango alisema hayo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma alipokuwa akifungua tawi la benki ya NMB wilayani humo na kusema kuwa bado huduma za kibenki vijijini ziko chini.

Alisema kuwa yapo maeneo wananchi wanatembea kwa umbali mrefu akitoa mfano wa kijiji Kilelema wilayani humo ambao walikuwa wakitembea kilometa 72 na Janda kilometa 95 kufuata huduma za benki wilayani Kasulu.

Alisema kuwa hali hiyo ilikuwa usumbufu mkubwa kwa wananchi hivyo kusababisha wananchi wengi kuhifadhi fedha zao ndani kwenye mitungi na kwamba pamoja na maendeleo ya kiteknolojia iliyofanya mitandao ya simu kutumika pamoja na mawakala wa benki lakini bado huduma za kibenki zipo chini.

Akielezea kuzinduliwa kwa tawi la NMB wilayani Buhigwe Makamu wa Rais alisema kuwa lina maana kubwa katika mchakato mzima wa maendeleo ikiwemo kusogezwa karibu kwa huduma karibu na wananchi na kwamba benki hiyo imeleta maendeleo makubwa nchini katika uwekezaji, utekelezaji wa miradi ya  maendeleo,mikopo kwa wakulima na wafanyabiashara.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Edwin Mhede alisema kuwa nia ya kufunguliwa kwa tawi hilo ni kusogeza  huduma karibu na wananchi katika wilaya hiyo mpya lakini yenye mahitaji makubwa ya huduma za kibenki  kutokana na shughuli za kiuchumi zilizopo.

Awali Kaimu Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema kuwa benki hiyo imeweza kufikisha matawi 229 nchi nzima na mashine za kutolea fedha 180 huku ikiwa na mawakala zaidi ya 20,000 na tawi Buhigwe lililofunguliwa linafanya mkoa Kigoma kuwa na matawi sita.

Mponzi ambaye amemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB,Ruth Zaipuna alisema kuwa kufunguliwa kwa tawi hilo kunalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kwa tawi la Buhigwe benki imetenga Sh bilioni 1 kwa ajili ya kutoa mikopo na tawi hilo litakuwa na huduma zote za kibenki kama matawi mengine nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button