MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameyataka mataifa ya Afrika kushirikiana kukabili changamoto zinazojitokeza katika bara hilo ili kuwa na usalama wa chakula.
Aidha, Dk Mpango alisema ajenda ya usalama wa chakula inapaswa kuendelea kujadiliwa katika mikutano mingine ikiwemo ya kikanda na Mkutano wa Umoja wa Afrika kwa sababu inagusa maisha ya kila siku.
Alisema hayo kwenye Jukwaa la Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika katika Kongamano la Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani barani Afrika Mwaka 2022 (AGRF 2022) linalofanyika Kigali, Rwanda.
Wajumbe wa jukwaa hilo walijadili namna nchi za Afrika zitakavyoweza kukabili tishio la usalama wa chakula kutokana na sababu mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabianchi, athari za Covid-19 na migogoro.
Dk Mpango alisema mataifa ya Afrika yanapaswa kuungana katika utumiaji wa rasilimali zilizopo ikiwemo nishati na gesi.
Alisema migogoro iliyopo katika mataifa mbalimbali barani Afrika inapaswa kukomeshwa ili kuruhusu wakulima waweze kuzalisha mazao kwa utulivu na amani.
Dk Mpango alisema serikali ya Tanzania inafanya jitihada kuinua sekta ya kilimo ikiwemo kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo.
Alisema kwa sasa kuna viwanda viwili kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea vinaendelea kujengwa, kuongezwa kwa bajeti ya sekta ya kilimo, kuanzisha skimu za umwagiliaji pamoja na ujenzi wa majengo ya kuhifadhia mazao.
Dk Mpango alisema pia serikali imeendelea kuboresha sera pamoja na jitihada za kuwawezesha wakulima kupata mikopo katika taasisi za fedha kwa riba nafuu na kuondoa kodi zaidi ya 140 miongoni ya zilizokuwa zikiwaathiri wakulima.
Aliwakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya kilimo nchini Tanzania ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula barani Afrika.