Dk Mpango ataka uwekezaji tafiti za kisayansi, teknolojia

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema ili kuinua viwango vya tafiti za vyuo nchini, vyuo vya elimu ya juu havina budi kuendelea kuwekeza katika tafiti hususan za sayansi na teknolojia na kuhimiza ubunifu katika ufundishaji na ujifunzaji.

Makamu wa Rais amesema hayo aliposhiriki Mahafali ya 27 ya Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) yaliyofanyika mkoani Iringa.

Advertisement

Ametoa wito kwa sekta binafsi kuunga mkono jitihada hizo kwa kuendelea kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu kwa kufadhili tafiti, kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani mbalimbali, kuanzisha vyuo vya elimu ya juu, kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo na mafunzo kazini.

SOMA: Jenerali Mabeyo Mkuu mpya Chuo Kikuu Iringa

Dk Mpango amesisitiza umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya elimu ya juu.

Amesema uwekezaji katika mifumo ya Tehama utawezesha ufundishaji wa baadhi ya masomo kwa njia ya mtandao na hivyo kuongeza idadi ya Watanzania watakaopata elimu ya juu.

Dk Mpango amesema ufundishaji kwa njia ya mtandao utapunguza changamoto ya uhaba wa walimu ambapo mwalimu mmoja anaweza kuwafikia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

Halikadhalika, ametoa wito kwa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, ili kufundisha masomo na ujuzi muhimu unaokosekana nchini pamoja na ujuzi wenye wataalamu wachache kama vile madaktari bobezi wa upasuaji wa neva, upandikizaji wa uroto, upandikizaji wa figo, uhandisi wa roboti, fizikia ya nyuklia, matumizi ya akili mnemba na teknolojia.

Vilevile amewasihi wahitimu kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini kama vile sekta za kilimo, biashara, ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, nishati jadidifu, matumizi ya teknolojia za kidijiti na Tehama, unenepeshaji wa
mifugo, ufugaji wa nyuki, biashara na viwanda vidogo ili kujipatia mitaji.

Aidha, amewahadharisha wahitimu kuhusu tabia ya kupenda mafanikio ya haraka pasipo kufanya kazi kwa bidii.

Amewasihi kupenda kufanya kazi, kuepuka njia rahisi, kuwa waadilifu na waaminifu.

Dk Mpango alipongeza jitihada za Kituo cha Ujasiriamali na Ubunifu na atamizi ya Kiota ya Chuo Kikuu cha Iringa kwa kutoa mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali kwa wanafunzi na wajasiriamali.