Jenerali Mabeyo Mkuu mpya Chuo Kikuu Iringa

MKUU wa Majeshi mstaafu, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amesimikwa rasmi kuwa Mkuu Mpya wa Chuo Kikuu cha Iringa akichukua nafasi ya Askofu Mstaafu Elinaza Sendoro aliyemaliza muda wake baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu.

Tukio hilo limefanyika leo katika mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo mjini Iringa huku zaidi ya wahitimu 1900 wakitunukiwa vyeti vyao katika fani mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya kusimikwa, Jenerali Mabeyo ameushukuru uongozi wa taasisi hiyo kwa kumpa nafasi hiyo muhimu kwa maendeleo ya elimu nchini huku akiahidi kushirikiana na uongozi na wadau wake wote kukitangaza vyema chuo hicho.

“Nashukuru kwa heshima hiyo mliyonipatia, nimeipokea na nimuombe mwenyezi Mungu aniongoze ili niweze kuwatumikia vyema wanajumuiya wa chuo hiki kwa manufaa ya jamii yote ya watanzania,” alisema Mabeyo.

Baada ya kupewa wadhifa huo, Jenerali Mabeyo naye amemteua Meja Jenerali Paul Kisesa kuwa mjumbe wa baraza la Chuo hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego kwa upande wake amewataka wahitimu hao kuwa mfano katika jamii kwa kusaidia kupambana dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

“Maambukizi ya VVU ni moja ya janga linalotishia vijana wetu kutokana na aina ya maisha wanayotaka kuyaishi. Ninyi ni wasomi tunajua mnazijua njia za kujiepusha na maambukizi yake lakini pia wasaidieni vijana wenzenu wengine wasitumbikie katika shida hiyo,” alisema.

Pia Dendego amewataka wahitimu hao kuwa kielelezo cha ubora kwa kutoa mapendezo au ushauri kwa serikali wa namna inavyoweza kupambana na tatizo la ajira nchini.

“Mimi binafsi kwa miaka minne iliyopita sikuwa na ajira; ajira yangu ya mwisho ilikoma mwaka 2017, nilivyorudi nyumbani nilisema sichagui kazi ya kufanya kwasabubu nilikuwa na maarifa yakutosha hivyo nilijiingiza katika ujasilimali na maisha yalienda,” alisema Dendego akiwasihi wahitimu hao kufikiria namna ya kujiajiri.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x