MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa siku 10 kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Mbeya wamalize ujenzi wa miundombinu ya ukaguzi wa magari katika eneo la Mlima wa Inyala mkoani Mbeya ili kukabili changamoto ya ajali mara kwa mara.
Dk Mpango pia ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikamilishe haraka barabara ya mchepuko katika eneo la Mlima wa Inyala Kijiji cha Shamwengo ili kupunguza matukio ya ajali katika eneo hilo.
Alitoa maagizo hayo jana alipotembelea eneo la Inyala mahali zilipotokea ajali mbili hivi karibuni ka kusababisha vifo vya watu wapatao 25.
Dk Mpango alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 2.5 ijengwe haraka kwa kiwango cha lami kurahisisha upishanaji wa magari katika eneo hilo.
Alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urich Matei asimamie ukaguzi wa magari yanayopita katika eneo la mlima wa Inyala ili kuepusha madhara ya ajali zinazojitokeza kutokana na ubovu wa magari.
Dk Mpango alisema serikali inasikitishwa na madhara ya ajali yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali na kuwataka wahusika likiwemo Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wao.
Alisema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ukiwemo upanuzi wa barabara inayopita mkoani Mbeya kuanzia Igawa hadi Tunduma mkoani Songwe.
Katika hatua nyingine, Dk Mpango wakati akiwasalimu wananchi wa Kijiji cha Shamwengo kilichopo kata ya Inyala alisema serikali itakamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho ulioanza kujengwa na wananchi kwa kutoa shilingi milioni 100 za umaliziaji na kuchimba kisima katika eneo hilo ili kusaidia upatikanaji wa huduma za maji.
Aliwapongeza wananchi hao kwa jitihada za kuanzisha mradi huo na moyo wao wa kujitolea katika kusaidia majeruhi wa ajali zinazotokea katika eneo hilo.