Dk Mpango: Tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kufanya kazi

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa vitendo ikiwemo kufanya kazi kwa bidii pamoja na kupinga vikali rushwa.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, wakati wa ibada maalum ya kumuombea Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki Mjini Bukoba, mkoani Kagera leo Oktoba 14, 2022.

Amesema katika kumuezi hayati Baba wa Taifa ni lazima kuendelea kusisitiza amani na umoja kwa Watanzania, pamoja na bara la Afrika kwa ujumla.

Advertisement

Aidha ametoa wito kwa viongozi kuendelea kufanya kazi kwa kutenda haki, kufanya kazi kwa uadilifu na kuondokana na rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Makamu wa Rais amewaasa Watanzania kufanya bidii katika masomo, ili taifa liweze kupata wataalamu watakaotoa msaada katika mambo mbalimbali nchini.

Ametoa wito kwa Watanzania kutafuta hekima za Mwenyezi Mungu wakati wote wa kutekeleza majukumu, kama alivyofanya hayati Baba wa Taifa enzi za uhai wake.

Ibada maalum ya Kumuombea hayati Mwalimu Nyerere imeongozwa na Askofu wa Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini na kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango pamoja na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango.

Wengine waliohudhuria ni familia ya Baba wa Taifa, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa Manyara, Makongoro Nyerere, mawaziri mbalimbali, Mkuu wa Mkoa Kagera , Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali, dini na vyama vya siasa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *