RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amesema atawasaidia wawekezaji wanaokumbana na vikwazo na changamoto mbalimbali.
Aliyasema hayo jana alipozungumza na wawekezaji wa kampuni mbalimbali za China waliofika kuzungumza naye kuhusiana na fursa za uwekezaji zinazopatikana Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Akizungumza na Mwenyekiti wa kundi la kampuni za Liyu Group, Yuefeng Wang wanaojishughulisha na utengenezaji viatu na kuzalisha umeme alisema nishati kwa sasa inahitajika zaidi Zanzibar kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya viwandani.
Kwa upande wa biashara ya viatu Dk Mwinyi aliwashauri wawekezaji hao kuangalia soko pana la Afrika.
Katika hatua nyingine alikutana na Quan Chen wa Kampuni iliyopo Tanzania, iitwayo Tanzania Binjiang inayoshughulika na usindikaji wa nyama na kumuarifu soko la nyama lipo kubwa na kusisitiza zifuatwe taratibu.
Dk Mwinyi pia alikutana na Xiaoli Zhou mwekezaji wa utalii wa michezo na alimkaribisha kuwekeza Zanzibar pamoja na kundi la wafanyabiashara wanawake kuitembelea Zanzibar.
Vilevile Dk Mwinyi alihojiwa na vituo viwili vikubwa vya China vinavyorusha matangazo kwa lugha ya Kiingereza ambavyo ni China Global TV Network na baadaye Shirika la Habari la China-XINHUA.
Comments are closed.