Dk. Mwinyi asisitiza umuhimu wa sayansi na Teknolojia
CUBA:Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi amesema Sayansi,Teknolojia na Ubunifu ni mambo muhimu kwa nchi zinazoendelea hasa katika masuala ya uchumi wa kijamii kwa vile nchi hizo zinaweza kubadili maisha ya watu wake kupitia sekta muhimu kama ya kilimo, nishati na elimu.
Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo alipohutubia katika Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Kundi la 77 pamoja na China akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan unaofanyika katika ukumbi wa mkutano, Havana Cuba.
Aidha Dk.Mwinyi amekumbusha namna nchi zinazoendelea zilivyoathirika vibaya na janga la UVIKO-19, kwa kupanda kwa bidhaa, mizozo ya kisiasa na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema hizo ni baadhi ya changamoto zilizosababisha kupanda kwa gharama za maisha na kudhoofisha jitahada za kujikwamua kiuchumi kwa nchi zinazoendelea.
Katika hotuba yake alikumbushia namna nchi zilizoendelea zilivyobania teknolojia ya kutengeneza chanjo nchi za mataifa ya kusini na kuzinyima kabisa msaada wa kiteknolojia ili ziweze kutengeneza chanjo, hali hiyo iliyosababisha makampuni ya utengenezaji dawa ya mataifa tajiri kujipatia faida kubwa kwa kuziuzia nchi masikini chanjo ya UVIKO-19.
Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi akazitaka nchi za kundi la G77 na China wachukulie hayo yote kama somo na zisibweteke kusubiri msaada kutoka mataifa tajiri, huu ndio wakati wa kusema imetosha.