Dk Nchimbi ashiriki mazishi ya Katibu wa CCM Kilolo

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi ameongoza waombolezaji katika shughuli ya kutoa heshima za mwisho na mazishi ya aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Christina Kibiki, ambaye alipoteza uhai hivi karibuni baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake na kupigwa risasi.

Balozi Dk Nchimbi aliyeambatana na Mjumbe wa Kamati Kuu, Haji Gavu, ambaye ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM -Oganaizesheni na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda wameungana na viongozi wa CCM wa ngazi mbalimbali mkoa wa Iringa na mikoa jirani na mamia ya waombolezaji katika mazishi hayo yaliyofanyika leo.

Kabla ya mazishi hayo yaliyofanyika nyumbani kwa katibu huyo katika Kijiji cha Banavanu, Tosamaganga, nje kidogo ya manispaa ya Iringa, Balozi Dk Nchimbi alijumuika pamoja na waombolezaji wengine katika ibada ya mazishi ya marehemu iliyofanyika katika Kanisa la Romani, Tosamaganga.

Advertisement

Akizungumza wakati wa mazishi hayo, Dk Nchimbi aliwasilisha salamu za rambirambi za Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk Samia Suluhu Hassan aliyesikitishwa na kuumizwa na kifo cha mchapakazi wa chama hicho.

“Tumeambiwa pamoja na risasi, walimvunja mikono na kumpiga kichwani. Bila shaka kifo cha kiongozi huyo kilikuwa cha maumivu makali sana. Inasikitisha ndugu yetu huyu kuuawa kinyama namna hiyo,” alisema.

Alisema mauaji ya namna hiyo hayakubaliki na kinyume na tabia ya watanzania na kama yakifumbiwa macho yanaweza kuzalisha hofu kubwa katika jamii na kuifanya iishi kwa woga.

“Napenda tutambue kwamba dhamana ya kwanza ya kujilinda ni ya kwako na pili kila mtanzania ana dhamana ya kumlinda mtanzania mwenzake, tusiishie kupiga picha na kusambaza mitandaoni matukio haya ya kinyama,” alisema.

Alisema CCM itatoa rambirambi zake na itakabidhi kwa watoto wa marehemu na kuendelea kuwa jirani na familia yao katika kipindi hiki kigumu.

Awali Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin alisema CCM Mkoa wa Iringa imepokea kwa mshtuko kifo cha kiongozi huyo.

“Tumesikitishwa na tunalaani sana tukio hilo. CCM mkoa wa Iringa ina imani serikali ina mkono mrefu, na kwamba wahusika watapatikana na sheria zitachukuliwa,” alisema

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba alisema kuna watu wamefanya makusudi kukatisha maisha ya kiongozi huyo wa CCM na ni jambo lililofanyika kinyume na utamaduni na maisha yetu kama watanzania.

“Serikali ipo kazini, inafanya uchunguzi ili tuwafahamu waliokatisha maisha ya kiongozi wetu. Kazi inaendelea na tunapata misaada kwa mikoa ya jirani ili wapatikane na wafikishwe mbele ya mikono ya sheria,” alisema.

Kibiki alipigwa risasi Novemba 12, mwaka huu katika tukio hilo la kikatili ambalo Jeshi la Polisi linaendelea kulichunguza ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahusika na watakapokamatwa watafikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Marehemu ameacha watoto watatu na wajukuu watano.