Dk Ndumbaro: Mji wa serikali una uhaba majengo ya sanaa

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,Dk Damas Ndumbaro amesema Mji wa Serikali Dodoma bado unachangamoto ya uhaba wa majengo ya sanaa na utamaduni na kuiomba Serikali ya China, kuongeza ushirikiano wake na Tanzania kwenye eneo hilo.

Dk Ndumbaro alitoa ombi hilo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam katika hafla ya Tamasha la Mavuna linaloadhimishwa katika utamaduni wa Kichina, lililoenda sambamba na kuadhimisha miaka 10 ya Mpango wa Ukanda Mmoja,Njia Moja (BRI) ambao Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayonufaika.

BRI ni mpango wa China kuzisaidia nchi za Afrika na nyingine zinazoendelea kuboresha sekta mbalimbali kama miundombinu,biashara na uwekezaji katika kuunganisha mataifa na kuboresha maisha ya watu wake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Ndumbaro alisema Serikali ya Tanzania na China walisaini Mkataba wa Makubaliano wa Utamaduni Aprili 30, mwaka 1992 na wakaendelea kuuhisha mwaka 2017-2020 na kisha mwaka 2022 -2025 na kuweka msisitizo kwenye eneo la Utamaduni na Sanaa.

Alisema katika kuendeleza sekta hiyo eneo la utamaduni bado kuna changamoto hususan katika mji wa Kiserikali wa Dodoma na kuiomba China iendelee kushirikiana na Tanzania ili kujenga kituo cha Taifa cha Utamaduni kitakachohifadhi na kuwa na masuala yote yanayohusu utamaduni wa Mtanzania.

“Tanzania ina uhaba wa majengo ya utadamuni hususan kwenye mji mpya wa kuresekali Dodoma, serikali inataka kujenga Kituo cha Taifa cha Utamaduni, tunaomba ushirikiano wenu kufanikisha hili,”alisema Dk Ndumbaro.

Aidha, alitaja eneo jingine la kipaumbele kuboresha sekta ya utamaduni,sanaa na michezo ni kutafuta wadau wanataosaidia kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wasanii na kazi za sanaa lakini pia wataalam wa fani hizo ili kuboresha uwezo na ujuzi wao katika kuimarisha sekta hiyo.

Eneo la tatu Dk Ndumbaro aliloomba wadau kushirikiana zaidi ni katika kuendeleza Lugha ya Kiswahili na kuwaomba China isaidie katika kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa ili lugha hiyo iendelee kupewa kipaumbele.

Alisema China ni marafiki wazuri wa Tanzania na wameendelea kuwa karibu kushirikiana katika nyanja mbalimbali za maendeleo kama vile biashara, uchumi, elimu na ujenzi wa miundombinu hivyo kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Chen Mingjian alisema katika kuadhimisha miaka 10 ya BRI, China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuleta maendeleo ya watu.

Alisema ushirikiano wa China na Tanzania unazidi kuimarika na hiyo inashuhudiwa pia na idadi ya Wachina iliyoko nchini na hata fursa za biashara, masomo na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa ushirikiano wa mataifa hayo mawili.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button