Dk Samia kuendelea na kampeni kesho Singida

SINGIDA: Mgombea kiti cha rais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk Samia Suluhu Hassan kesho anatarajia kuanza kunadi sera zake kwa wananchi wa Singida katika maeneo ya Manyoni, Ikungi na kumalizia Singida Mjini.
Safari hii ya kampeni inakuja baada ya Samia kukamilisha kampeni katika mikoa ya nyanda za juu kusini, mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa ambao alibainisha sera zake kwa maelefu ya wananchi waliokuwa wakifurika kwenye mikutano yake akitumia karata ya kubainisha mafanikio ya serikali yake na ahadi kwa miaka mitano ijapo pindi wananchi watampa ridhaa ya kuunda serikali.
Katibu wa CCM, Mkoa wa Singida, Lucy Boniface anasema maandalizi kwa ajili ya mikutano hiyo yako vizuri na watampokea katika Wilaya ya Manyoni na kuelekea Ikungi na kisha atamalizia mkutano mkubwa katika uwanja wa Bombadia Singida Mjini
“Tumejipanga kumpokea kwa bashasha kubwa kwa vikundi vya hamasa wasanii na watu wengi wapo tayari kuhakikisha Mkoa wa Singida tunaweka historia,”alisema Katibu huyo wa CCM Mkoa.
Amesema siku inayofuata ataelekea Wilaya ya Iramba ambako atafanya mkutano mkubwa katika eneo la Misingiri na kisha kuelekea mkoani Tabora.



