Dk. Sule: amani muhimu kuliko madaraka

MWENYEKITI wa Taasisi ya Islaah Islamic, Dk. Seif Sule maarufu kama Dk. Sule ametoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanalinda amani ya taifa kwa gharama yoyote, hasa wakati huu ambapo nchi inajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dk. Sule amesema historia ya Tanzania katika chaguzi nyingi za vyama vingi imeonyesha ukomavu wa kisiasa, licha ya changamoto ndogo ndogo ambazo hazikuwahi kuhatarisha amani ya taifa.
Hata hivyo, alionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya sasa ya kisiasa, akisema kuna viashiria vinavyoashiria kuvunjika kwa utulivu wa kitaifa.
“Tunapoangalia mitandao ya kijamii na kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa, hasa wale wanaotaka madaraka kwa njia yoyote, tunaona wazi kuna hatari inayokuja. Hawa ni watu wanaotaka uongozi kwa gharama yoyote jambo ambalo Watanzania hatupaswi kukubaliana nalo kamwe,” amesema Dk. Sule.
Akitumia mfano wa historia ya chaguzi nchini, Dk. Sule alikumbusha kuwa tangu mwaka 1995 hadi sasa, vyama vya upinzani vimewahi kupata mafanikio makubwa kwa kutumia hoja, sera na mikakati ya kisiasa. Alisema ushindani wa hoja ndio msingi wa siasa safi, siyo fujo wala chokochoko za kuchochea vurugu.
“Upinzani wa kweli ni ule unaoibua hoja mbadala kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Siyo kuvunja Katiba, siyo kuhamasisha maandamano ya vurugu au kutoa kauli zinazohatarisha utulivu wa taifa,” amesisitiza.
Kwa sauti ya masikitiko, Dk. Sule alizungumzia mwenendo wa baadhi ya viongozi wa upinzani, akimtaja wazi Tundu Lissu wa CHADEMA, kwamba kauli zake kama “No Election, No Reform” siyo tu zinakinzana na Katiba bali pia ni hatari kwa mshikamano wa kitaifa.
“Kauli hiyo inaashiria uasi. Katiba yetu inasema uchaguzi lazima ufanyike. Unapohamasisha watu wakatae uchaguzi, maana yake unawataka wavunje sheria. Huo siyo uzalendo, huo ni uchochezi,” amesema Dk. Sule.
Aidha, alieleza kuwa amani ya Tanzania imedumu kwa miongo mingi na ndiyo msingi wa mafanikio ya nchi. Alitoa mfano wa nchi jirani na zile za Afrika ya Kati kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako watu huishi kwa hofu kutokana na machafuko ya kisiasa ya muda mrefu.
“Nina marafiki wanaoishi Goma, DRC. Wao wanakutana na maiti kila siku, hawalali usiku. Watanzania tusisubiri tufike huko ndipo tuanze kuthamini amani,” alionya.
Amewaasa Watanzania kuwa makini na siasa zenye ajenda binafsi. Amesema baadhi ya viongozi wanaochochea vurugu wana familia zao nje ya nchi, huku wananchi wa kawaida wakiwa ndio waathirika wa moja kwa moja.
“Mtu wa kawaida wa Rufiji, Nzega au Tandahimba hana uwezo wa kukimbilia Ulaya. Akiharibu nchi yake, hana pa kwenda. Hili ni la msingi sana kulielewa,” amesema..