Dk Suleiman Haji akutana na ujumbe Tz mkutano CSW Marekani

KAIMU Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa NewYork nchini Marekani Balozi Dk Suleiman Haji Suleiman amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoshiriki mkutano wa masuala ya Maendeleo ya Wanawake CSW Makao Makuu ya UN New York.
Mkutano huo unaoenda sambamba na kusherehekea miaka 30 ya mafanikio tangu kufanyika kwa Mkutano wa Wanawake Beijing China mwaka 1995.

Katika mazungumzo hayo yaliyifanyika katika ofisi za uwakilishi wa Tanzania jijini New York na kuhudhuriwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia (Wanawake) na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar he Riziki Pembe Juma, Katibu Mkuu wa Mkutano wa Wanawake Beijing mwaka 1995 Mhe Balozi Gertrude Mongela, Mshauri wa Rais Masuala ya Jamii, Sophia Mjema, Naibu Katibu Mkuu Ardhi, Lucy Kabeyerwa na viongozi wengine wa serikali na asasi za Kiraia kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni washiriki wa Mkutano huo.
Mapema akiwakaribisha wageni hao, Balozi Dk Suleiman ameshukuru wajumbe hao kwa kushiriki kwa wingi katika mkutano huo muhimu unaokutanisha makundi mbali mbali ya viongozi wanawake kutoka serikali ulimwenguni na asasi za kiraia unaojadili masuala mbali mbali ya maendeleo ya wanawake na changamoto wanazopitia na namna ya kuzitatua.

Balozi Suleiman amewahimiza wajumbe wao kuweka maslahi ya nchi mbele katika ushiriki wao wakati wa majadiliano ili kuielezea sifa nzuri Tanzania katika medani sa Kimataifa na kuwaasa kutosita kuelezea maendeleo ya mwanamke wa kitanzania kutoka 1995 hadi leo 2025 ambapo dunia imeshiuhudia maendeleo makubwa ya mwanamke wa Kitanzania na dunia kwa ujumla.
Kwa upande Waziri Dk Dorothy Gwajima kwa niaba ya Ujumbe wa Tanzania ameushukuru Uongozi wa Ubalozi wa Tanzania NewYork na hasa Balozi Dk Suleiman kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo kwa ujumbe wote wa Tanzania unaoshiriki mkutano huo.

Pamoja na mkutano huo, Uwakilishi wa Tanzania New York uliandaa futari kwa ajili ya wageni hao ikiwa ni sehemu ya kuwakirimu wageni hao.Mkutano wa CSW unafanyika kila mwezi Machi ya kila mwaka na mwaka huu unafanyika kuanzia Machi 10 hadi Machi 22 jijini New York.



