Dodoma Jiji FC yapata mdhamini msimu mpya wa ligi

SHINYANGA: KAMPUNI ya Jambo Food Products (JAMKAYA ) imeeleza kusaidia vijana katika kukuza michezo nchini baada ya kutia saini mkataba wa mwaka mmoja na kutangaza rasmi kudhamini klabu ya Dodoma Jiji FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2025/2026.
Mkataba huo umesainiwa leo Septemba 23, 2025 kati ya viongozi wa Jambo Food Products na Dodoma Jiji FC, katika ofisi za kampuni hiyo Mkoani Shinyanga.

Msimamizi wa Chapa na Ubunifu wa Jambo Group, Nickson George akisaini mkataba huo amesema kampuni hiyo imeendelea kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo na kuzisaidia timu mbalimbali nchini, na sasa imeamua kuishika mkono Dodoma Jiji FC ili kufanikisha ndoto na malengo yao kwenye Ligi Kuu.
“Hatua hii siyo tu udhamini, bali ni ushirikiano wa kibiashara na kijamii utakaosaidia kukuza chapa za pande zote mbili kupitia michezo. Dodoma Jiji FC sasa ni sehemu ya familia ya Jambo Group – ‘Jamukaya’, na Jambo Group ni sehemu ya Dodoma Jiji FC,” amesema George.

Kiongozi wa Dodoma Jiji FC, Dickson Kimaro, ameishukuru Jambo Group kwa kuiamini timu yao na kuahidi kuitangaza vyema chapa ya kampuni hiyo kupitia matokeo mazuri katika msimu huu wa ligi.



