DP World yamaliza foleni bandarini

JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) imesema uwekezaji uliofanywa na serikali katika Bandari ya Dar es Salaam, umekuwa na ufanisi mkubwa kiasi cha kuondoa kabisa foleni ya muda mrefu ya meli zilizokuwa zikisubiri kuingia gatini kushusha mizigo.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo taifa, Hamisi Livembe amewaambia waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa uwekezaji wa Kampuni ya DP World na Adan Ports umesaidia pia kupunguza muda wa kuhudumia makasha bandarini hapo kutoka siku 10 hadi siku tatu.

Livembe aliyeongoza ujumbe wa JWT kutembelea bandari hiyo kujionea ufanisi wa sasa ikilinganishwa na
kabla ya uwekezaji huo.
Kutokana na vifaa vya kisasa vya mwekezaji, meli zote zinazoingia zinahudumiwa bila kukaa foleni.
SOMA: DP World itashusha gharama Bandari ya Dar es Salaam
“Kama mnavyojua malalamiko ya wafanyabiashara Kariakoo mwaka juzi yalihusu kuchelewa kuhudumia meli ambapo meli zilikuwa zikikaa foleni kwa siku hadi 30 na hata zikiingia gatini zinachukua siku 10 hadi 15 kuhudumiwa hali iliyosababisha mizigo na bidhaa kupanda bei,” amesema.

Amefafanua kuwa bei za bidhaa zilipanda kwa sababu gharama za kuhudumia kasha moja zilipanda kutoka dola za Marekani 3,000 hadi 8,000 hali iliyosababisha mizigo mingi inayoenda Kariakoo kupanda bei.
Ameongeza kuwa pamoja na kusikia ufanisi huo wa bandari, waliona ni vema kwenda kujiridhisha na waweze kutoa taarifa kamili kwa wafanyabiashara ili wale waliokimbia kutokana na changamoto hizo wajue kuwa sasa ni wakati
mwafaka kurudisha mizigo Bandari ya Dar es Salaam.
“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa yametokea na bado wanaendelea na uwekezaji, tunaona mashine kubwa mbili za kushusha mizigo na bado wanaleta mashine nyingine ya tatu,” ameongeza.
Amesema mashine hizo mbili zinashusha makasha 1,000 kwa siku na sasa mwekezaji anafunga mashine ya tatu ya kushusha mizigo, hivyo ufanisi utaongezeka hadi makasha 1,500 au 2,000.

Amesema meli nyingi zinazokuja bandarini zina makasha 3,000 hivyo zinahudumiwa ndani ya siku tatu.
“Kwa niaba ya wafanyabiashara wote, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu wenye faida kwa Watanzania na kutokana na ufanisi huu, bei ya kuhudumia kasha imeshuka kutoka Dola za Marekani 8,000 hadi 3,000 ambayo ni bei ya mwanzo,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abeid Gallus amesema ujio wa wawekezaji katika bandari hiyo umeleta mafanikio makubwa na muda wa meli kusubiri nje umepungua kutoka zaidi ya siku 30 hadi siku sifuri.
Ameongeza kuwa muda wa kuhudumia shehena kwenye meli zikiwa gatini umepungua kutoka siku zaidi ya 10 hadi siku tatu na kuleta mchango chanya katika biashara za Tanzania ndio maana JWT imeamua kuja kushuhudia.
Amesema mbali na ufanisi wa bandari, machafuko ya Msumbiji yamesababisha mizigo iliyokuwa ikipitia Bandari ya Beira sasa inapitia Bandari ya Dar es Salaam na kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea kufanya tathmini kujua mzigo huo ni kiasi gani na taarifa itatolewa.
Meneja Mahusiano wa Kampuni ya DP World Tanzania, Elituno Malamia alisema tangu Mei 2024 walipoanza kufanya kazi hadi sasa, wameweza kuhudumia kwa asilimia 25 zaidi ya hali ilivyokuwa awali.
Amesema kwa Desemba walivunja rekodi ya bandari ambapo walihudumia magari 25,251 na meli 16 za magari ndani ya mwezi mmoja ikilinganishwa na magari 12,500 na meli saba katika kipindi kama hicho mwaka juzi.
“Hicho ni kiwango kikubwa na tunajivunia kutokana na kazi hiyo. Changamoto ambayo tunapitia ni kwa watu kuchelewa kuondoa mizigo yao katika vituo vya kuhifadhia mizigo (ICD),” amesema Malamia.
Amesema kulingana na takwimu zilizopo, mwaka 2024 waliweza kuhudumia makasha milioni moja kwa mwaka ikilinganishwa na 255,000 kwa mwaka kabla ya uwekezaji wao.



