Dume moja majike matatu kwa mazao tarajiwa ya Samaki

Soko la nje la Samaki

DUME moja la samaki linapaswa kuhudumia/kuzalisha majike matatu tu katika bwawa ili mfugaji apate mazao tarajiwa, kwa maana ya ubora.

Na wazazi hao wakifanya kazi ya kuzaliana kwa awamu nne mfululizo, wanapaswa kupumzika kwa muda wa miezi miwili ili kurudisha nguvu walizopoteza katika mchakato wa uzalishaji.

Kila jinsi itakuwa na bwawa lake la mapumziko hadi watakapounganishwa tena kwa ajili ya kuendelea na kazi ya kuzaliana.

Advertisement

Awamu moja ya kuzaliana inachukua takribani siku 21 baada ya mayai kupevuka, ambapo jike atatema kwenye eneo waliloandaa wazazi wenyewe kwenye bwawa, ili dume ayarutubishe.

“Jike akishatema mayai dume atapita kuyamiminia manii. Ndio maana ni lazama wote waende mapumziko kwa sababu wamechangia nguvu kubwa katika mchakato wa kuzaliana, kulingana na majukumu ya kila mmoja,” anasema Msimamizi wa utotoleshaji vifaranga katika shamba la samaki ‘Son Fish Farm’, jijini Jinja nchini Uganda, Joseph Nsenga.

Alitoa elimu hiyo hivi karibuni wakati wa ziara ya maofisa na wafugaji samaki wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, waliotembelea shamba hilo kupata ujuzi zaidi.

Ziara hiyo iliratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda kwa kushirikiana na Shirika la Samaki Ziwa Victoria (LVFO).

Nsenga anasisitiza kwamba samaki wazazi wazaliane mara nne kabla ya kwenda mapumziko hayo ya miezi miwili na kuzaliana kufanyike ndani ya miezi 24.

Baada ya hiyo miaka miwili wanapaswa kupumzika ili wasije wakazaa watoto dhaifu kwani wanakuwa wamechoka.

Shamba hilo linalofuga samaki aina ya sato peke yake linatotolesha vifaranga katika mabwawa na kisha kuvihamishia kwenye vizimba katika Ziwa Victoria, vinapotimiza uzito wa gramu moja.

Kwa sababu za kiuchumi zinazohitaji mazao bora, uzalishaji samaki katika shamba hilo unazingatia kanuni hiyo ya ‘dume moja majike matatu’ lakini pia kuzalisha madume wengi kwani ndiyo yenye soko kubwa ikilinganishwa na majike.

Katika kulifanikisha hilo, wataalamu wa shamba hilo wanatumia teknolojia ya kubadili jinsi ya samaki, maarufu kama ‘sex reversal’ kupata madume tarajiwa.

Nsenga anasema kawaida samaki anazaliwa bila jinsi, isipokua msukumo wa kuwa dume au jike unategemea mazingira wanayokulia viumbe hao.

“Sasa sisi tunawalisha vyakula vyenye homoni za kiume baada ya kutotolewa na tunapata madume ya kutosha,” anasema.

Sambamba na vyakula vyenye homoni za kiume, madume yanakuwa bora kwa sababu ya kuzingatia uwiano wa dume na majike wakati wa kuzaliana.

Madume yana soko kubwa kutokana na kukua haraka pamoja na kuwa na uzito mkubwa ikilinganishwa na majike.

“Hata mwonekano wake, unavutia kuliko wa samaki jike,” anasema mtaalamu huyo.

Sababu mojawapo ya jike kuwa na uzito mdogo ni kutokuwa na muda wa kutosha kula, hasa kipindi cha kuzaliana.

Katika kipindi hicho, jike hulazimika kuyameza mayai yaliyokwisharutubishwa ili yapate joto la kupevuka na kutotolewa haraka.

Sababu nyingine ya kumeza mayai ni usalama, kwani muda mwingi mama anakuwa na wasiwasi wa kupokonywa na maadui.

“Anayatema mara moja moja, tena kwa muda mfupi ili kupata chakula na kisha kuyameza tena. Kwa hiyo unaweza kuona ni kiasi gani anakosa muda wa kula vizuri,” anasema Nsenga.

Anazungumzia zaidi upatikanaji wa mazao bora ya samaki kwamba baada ya vifaranga kutotolewa, vihamishiwe kwenye bwawa lingine ili kuwapa nafasi nzuri wazazi ya kuendelea kuzaliana.

Kuhamishwa haraka pia ni kwa ajili ya kuanza mchakato mapema wa kuzalisha madume ya kutosha kupitia ‘sex reversal’.

Kabla ya vifaranga kuhamishiwa ziwani, madume na majike maalumu kwa ajili ya kuzaliana wanachaguliwa na kuhamishiwa bwawa lingine kwa maandalizi ya kazi hiyo inayoanza wakiwa na umri wa miezi mitatu.

Wengine wataachwa kwa wiki tatu ili watimize uzito unaotakiwa, kisha wanahamishiwa kwenye vizimba vya samaki vijana (juvenile cage).

Wanakaa humo kwa miezi miwili ili watimize uzito wa gramu 20, ndipo wahamishiwe kwenye vizimba vya kukuzia na kuvunwa.

Mtaalamu anasema katika vizimba vya kukuzia samaki wanalishwa mfululizo ili kuhakikisha wanakuwa na uzito wa gramu 500 na zaidi ndani ya miezi sita, ambacho ndicho kipindi cha mavuno.

Ili kuepuka magonjwa ya samaki, mfugaji anapaswa kusafisha bwawa kila anapotaka kuweka mazao mapya.

Afungulie mabomba ya matoleo ya maji kuliacha bwawa tupu ili alisafishe kwa dawa, hasa aina ya ‘chroline 90’.

Yajazwe maji upya ya kuondoa hiyo dawa na bwawa likae tupu kwa muda wa japo siku tatu kabla ya kuweka mazao mapya.

Endapo ni kwa ajili ya kuzaliana, dimbwi lijazwe kwanza michanga kabla ya maji kwani wazazi huchimba mashimo kwenye michanga hiyo kwa ajili ya kuweka mayai.

Tafiti zisizo rasmi zinasema ili samaki dume atimize majukumu yake ipasavyo, anapaswa kumkuta jike kwenye bwawa. Akitangulia yeye na kukuta hakuna mwenyeji, basi jike akiletwa dume atasusa.

Watanzania walipata pia fursa ya kutembelea vizimba vya shamba hilo ndani ya Ziwa Victoria huku Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dk Aziz Mlima akiomba wataalamu hao kuja Tanzania kuwapatia mafunzo wafugaji wengi kwa pamoja.

Mkurugenzi wa Shamba hilo, Robert Osinde, anasema wataalamu wako tayari kubadilishana ujuzi na Watanzania wakati wowote, ili kukuza uchumi wa nchi hizo kupitia sekta ya uvuvi.

Anasema ni muhimu wafugaji kupata elimu ya kutosha kabla ya kuanza uwekezaji, hasa ikizingatiwa kwamba ufugaji samaki unahitaji mtaji mkubwa.

Anasisitiza ubadilishanaji wa ujuzi na maarifa ili wananchi wa nchi hizo mbili wanufaike na fursa za kijamii na kiuchumi zilizomo kwenye ufugaji samaki, ikiwemo ajira.

“Hadi sasa sisi tumetoa ajira kwa watu 136. Tuna vizimba 78 na kila kizimba kinazalisha tani 60, mara mbili kwa msimu. Masoko ni mengi ndani na nje ya nchi, hasa Kenya na Congo DR,” anasema Osinde.

Anasisitiza kuwa kama ambavyo uchunguzi wa awali unaonesha idadi ya watu katika nchi hizo mbili kuongezeka na uchumi kukua, vivyo hivyo mahitaji ya samaki, hivyo akahimiza kuwekeza katika eneo hilo lenye uhakika wa mavuno endapo mfugaji atafuata kanuni.

Hakuna haja ya Watanzania kuwekeza fedha kubwa kwenye ufugaji samaki lakini wakaambulia hasara kwa sababu tu ya kukosa ujuzi na maarifa wakati wataalamu wa shamba hilo wapo.

Kwa upande wa maji ya Ziwa Victoria anasema hana wasiwasi nayo kwani kwa asili ni masafi na yana joto linalotakiwa kuendesha shughuli hizo za ufugaji samaki.

Hata hivyo, Osinde anasema chakula cha samaki bado ni changamoto kwani kilicho bora kinaagizwa nje ya nchi. Kinachozalishwa ndani hakina ubora kutokana na kukosa virutubishi.

Katika uzalishaji mzima, ambao unachukua si chini ya miezi nane toka kupandikiza vifaranga, asilimia zaidi ya 70 ya uendeshaji inakwenda kwenye chakula kutokana na upatikanaji kuwa haba na gharama kubwa.

“Njooni kwetu mjifunze muda wowote milango iko wazi au wasiliana nasi popote mlipo. Hapa ndipo vinapopatikana pia vifaranga bora, chukueni mbegu,” anashauri Osinde.