KONGAMANO la Akili Mnemba linalotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2025 litashirikisha mataifa mbalimbali duniani pamoja na washiriki zaidi ya 1,000.
Hii ni fursa kubwa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kuinua na kuboresha kiwango cha sayansi na teknolojia hususani eneo la Akili Mnemba (AI) limeonekana kuvutia mataifa mengi duniani kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Wakati akikagua maendeleo ya maandalizi ya Mji wa Kigali ambako kongamano litafanyika, Rais wa Jukwaa la Uchumi wa Dunia (WEF), Børge Brende ameisifu Rwanda kwa namna ilivyojizatiti katika maandalizi ya kufanyika kwa Kongamano la Akili Mnemba linalotarajiwa kufanyika katika mji huo.
Brande alisema kufanikiwa kwa Rwanda ni mafanikio ya nchi zote za Afrika Mashariki na kuzitaka zijiandae kikamilifu kufanikisha kongamano hilo na kuionesha dunia kuwa Afrika Mashariki inaweza na iko tayari.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Kituo cha Mapinduzi ya Nne ya Viwanda cha Rwanda kwa ushirikiano na Jukwaa la Dunia la Kiuchumi, linatarajiwa kushirikisha mataifa zaidi ya 100 na washiriki zaidi ya 1,000 na kwamba ni fursa kubwa kwa wananchi wa Rwanda na Afrika Mashariki kwa ujumla, Tunaipongeza Rwanda kwa kuliwakilisha Bara la Afrika hususani Afrika Mashariki vizuri na kuionesha dunia kuwa Afrika Mashariki iko tayari na inaweza.
Ni vema nchi zote za Afrika Mashariki zikajipanga kushiriki katika jukwaa hilo kwa sababu ni fursa adhimu ya kukuza sayansi na teknolojia na pia maandalizi makubwa na muhimu kuelekea katika matumizi ya teknolojia ya akili mnemba katika nyanja mbalimbali.
Ni kweli kuwa matumizi ya akili mnemba yana faida kubwa katika jamii lakini pia yana hasara pia kama nchi washirika hazitachukua tahadhari ya kutosha kwa namna dunia inavyoelekea katika teknolojia hiyo.
Tunajua kuwa moja ya faida ya matumizi ya teknolojia ya akili mnemba ni kurahisisha kazi katika eneo husika na kuondoa foleni zisizo na maana. Mfano, matumizi ya teknolojia hiyo katika hospitali zetu inaweza kusaidia kurahisisha huduma kwa wagonjwa.
Pamoja na faida hizo, teknolojia hiyo ina hasara zake ikiwa ni pamoja na kupunguza watu katika sekta ya ajira na kusababisha umasikini kwa wananchi.
Hivyo, tunashauri wakati EAC ikiendelea kuisogelea teknolojia hiyo ihakikishe kuwa nchi wanachama wamechukua
tahadhari ya kutosha ili wananchi wake wasipoteze fursa za ajira ambazo ndio utajiri wa kwanza katika nchi husika.
Endapo uchumi katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki utashikiliwa na teknolojia ya akili mnemba, kutakuwa na hatari kwa wananchi ikiwa hawakuandaliwa vya kutosha kukabiliana na teknolojia hiyo kubwa iliyotingisha dunia.
Ikiwa tahadhari zote zitachukuliwa hususani kuwaandaa wananchi kukabiliana na teknolojia hiyo, hakutakuwa na
madhara yoyote kwa wananchi na uchumi wao utakua badala ya kushuka.