EAC iwekeze zaidi mahitaji ya wananchi

WAASISI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) bila shaka walikuwa na dhamira na shabaha kubwa ya kuunda muungano wa mataifa matatu, baadaye matano na sasa manane.
Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliwashawishi viongozi wenzake, Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya na Dk Milton Obote wa Uganda kwa pamoja walidhamiria kuwafanya wananchi wa mataifa hayo kwanza wawe na muingiliano kurahisisha biashara, uwekezaji na kuimarisha utamaduni wao unaokaribia kufanana.
Muingiliano huo umejengwa katika itifaki nne ambazo walitarajia taratibu kuiunganisha jumuiya hiyo kuwa kitu kimoja kwa kuwa na serikali moja.
Itifaki hizo ni pamoja na kuwa na umoja katika kutekeleza ushuru wa forodha, soko la pamoja, sarafu ya pamoja na mwisho kuwa na shirikisho moja la kisiasa ambapo EAC itakuwa na serikali moja.
Pamoja na hayo yote mahitaji ya wananchi wa EAC ni kurahisishiwa ushiriki wao katika biashara na uhakika wa kulindwa katika masoko ambapo wanaweza kuuza bidhaa zao kulingana na sheria zinazounda EAC.
Hili ndilo la msingi sana na ndilo lengo mama la uundwaji wa jumuiya hii kubwa Afrika na ambayo inatajwa kuwa ni jumuiya ya pili yenye nguvu kisiasa na kiuchumi baada ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU).
Kama tunakubaliana kuwa lengo mama la EAC ni kuwarahisishia wananchi katika shughuli zao za kibiashara na uwekezaji, tunatarajia kuona lengo hilo likitekelezwa katika nchi zote nane ili kuwezesha biashara kwenda vizuri bila kuvunja sheria.
Hatutegemei kuona nyongeza ya ushuru wa forodha kwa bidhaa zozote unaokwenda kinyume na makubaliano
yanayosimamiwa na Sekretarieti ya EAC.
Hatutegemei kuona bidhaa zikikwamishwa sokoni kwa visingizio ambavyo havipo katika sheria za utekelezaji wa itifaki za jumuiya.
Kumezuka kasumba ya baadhi ya nchi ndani ya EAC kuzuia baadhi ya bidhaa zikitaja malengo ya vitendo hivyo kuwa ni kulinda bidhaa za ndani dhidi ya bidhaa za nje zinazoingia katika nchi husika.
Vitendo hivyo vinastahili kukemewa kwa nguvu zote na kutajwa wazi ni kwenda kinyume na sheria na kanuni za
uundwaji wa EAC.
Tunasihi nchi zote zilizotia saini Mkataba wa Afrika Mashariki kuhakikisha zinaweka soko wazi kwa wafanyabiashara na bidhaa kutoka nchi zingine kama itifaki inavyotaka.
Tunazipongeza nchi zote za EAC ambazo zinatekeleza kwa uwazi itifaki zilizoiunda.
Ni matumaini yetu hata katika zile itifaki ambazo hazijatekelezwa kama sarafu ya pamoja na shirikisho la kisiasa ndani ya EAC zitaharakishwa ili wananchi wafaidi matunda ya mawazo ya waasisi wa jumuiya hiyo.



