EACOP, mkandarasi wafadhili masomo Watanzania 80

MRADI wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kushirikiana na mkandarasi wa kusambaza mabomba, umefadhili mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vijana Watanzania 80.

Mafunzo hayo yatatolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ili kuwapa ujuzi utakaowawezesha kupata fursa za ajira katika ujenzi wa mradi huo.

Meneja wa rasilimali zinazopatikana ndani ya nchi, Neema Kweka alisema hayo katika Chuo cha Veta Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango huo.

Kweka alisema ufadhili huo ni kielelezo cha kujitolea kwa mradi wa EACOP katika kutekeleza sera ya matumizi ya rasilimali za ndani kwenye mradi kwa kuwapa fursa wazawa.

“EACOP tunaendelea kutekeleza sera hii kwa kununua huduma za ndani, kutoa ajira, kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo wazawa, ikiwemo kuwapa nafasi ya kupata ujuzi kupitia mafunzo na wakandarasi wa kimataifa waliopo katika mradi,” alisema.

Aliongeza: “Ndiyo maana mkandarasi wetu, PCK wamefadhili mafunzo haya kwa vijana 80 kutoka vituo vya Veta Moshi, Shinyanga na Kilindi.”

Kweka alisema programu hiyo itafanyika kwa miezi 12 na mafunzo yatahusu fani mbalimbali ukiwemo ufungaji wa mabomba na mitambo, ujenzi na ufyatuaji wa matofali, ufungaji wa umeme, ufundi chuma na uendeshaji wa mitambo.

“Baada ya mafunzo haya, wahitimu watapewa vyeti vitakavyowawezesha kukubalika katika soko la ajira la kimataifa, ikiwemo kufanya kazi katika mradi wa EACOP, miradi ya kimkakati ya Serikali na hata kujiajiri wao wenyewe,” alisema.

Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Idara ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Gloria Njau alishukuru mradi wa EACOP kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha Watanzania hususani vijana wanapata ujuzi wa fani mbalimbali kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi.

“Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo, hivyo mpango huu wa mradi wa EACOP utazalisha wataalamu wengi katika fani mbalimbali na kuwa tegemeo katika ujenzi wa nchi,” alisema Njau.

Mkuu wa Chuo cha Veta Moshi, Lupakisyo Mapamba alisema kupitia ufadhili huo, chuo hicho kimetoa vijana 50 wakiwemo wasichana tisa watakaopewa mafunzo katika sekta ya mafuta na gesi.

Mapamba alisema ufadhili huo umehusisha vituo vya Veta Shinyanga chenye wanafunzi 20 na Veta Kilindi chenye wanafunzi 10.

Mmoja wa wanufaika wa ufadhili huo, Habiba Omary alisema mchakato wa kuwapata washindi ulikuwa wa wazi na wa haki.

Mnufaika mwingine wa programu hiyo, Emanuel Msangi alisema zaidi ya vijana 1,849 walishiriki kwenye usaili.

Mradi wa EACOP una urefu wa kilometa 1,443 kuanzia Hoima, Uganda hadi Peninsula ya Chongoleani katika Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kusafirisha mafuta ghafi kwenda kwenye soko la kimataifa.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button