DAR ES SALAAM: MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Aneth Komba amesema kuwa Mitaala mipya imefanyiwa maboresho ambapo elimu ya awali yaani chekechea itakua ni mwaka mmoja.
Amesema maboresho hayo ni makubwa na ya sita tangu nchi ipate uhuru.
Akifafanua amesema maboresho ya muundo wa elimu na hasa elimu ya awali itatolewa kwa muda wa mwaka mmoja kwa watoto wenye umri wa miaka mitano ambapo elimu ya awali itatanguliwa na elimu ya malezi na makuzi itakayotolewa kwa miaka miwili.
Dk Aneth ameyasema hayo leo Novemba 13,2023 katika ufunguzi wa mafunzo ya Wawezeshaji Kitaifa wa Mtaala wa Elimu ya Awali.
Amesema, kwa watoto wenye umri wa miaka mitatu mpaka minne, elimu hiyo itasimamiwa na wizara inayosimamia ustawi wa watoto ambayo kwa sasa ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia insia ,Wanawake na Makundi Maalum.
Amesema yapo maboresho yaliyofanywa kwenye maeneo ya ujifunzaji ambapo kwa sasa mtaala una maeneo makuu matano ambayo ni Utamaduni, elimu ya imani, sanaa na michezo, Lugha na mawasiliano.
Mitaala mingine ni Stadi za awali za maisha, Afya na mazingira, Stadi za awali za kihisabati, Kisayansi na TEHAMA.
Nae, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Tecknolojia, Dk Franklin Rwezimula amewataka wawezeshaji kitaifa wa mtaala wa Elimu ya Awali nchini kuzingatia mafunzo kwa umakini ili kuwawezesha walimu kutekeleza mtaala huo kwa weledi.
Mtaala huo unaotarajia kuanza mwaka 2024 kwa ngazi ya elimu ya awali na msingi.
“ Ili mitaala itekelezwe kwa ufanisi ni lazima kuwe na walimu wenye weledi katika ufundishaji, naomba sana wawezeshaji mzingatie haya mafunzo mnayopatiwa hapa ili muweze kuifanya kazi yenu ya uwezeshaji vyema” amesema, Dk Rwezimula.
Amesema Wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha mafunzo endelevu kazini ili kuhakikisha walimu wanakuwa bora katika maeneo yao ya kazi, ikiwemo uboreshaji wa mazingira katika miundombinu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia vikiwemo vifaa vya TEHAMA.
Comments are closed.