Elimu ya Ebola yafikishwa sokoni, gesti Kagera

KAMPENI za kujikinga na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mkoani Kagera zimeingia katika hatua nyingine baada ya Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kuanza kupita nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu, mtaa kwa mtaa kwa lengo la kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Dk Ama Kasangala amekuwa akitembea kwa miguu mitaani, sokoni na nyumba za kulala wageni kuhakikisha elimu ya namna ya kujikinga na Ebola inawafikia kwa wengi.
Akizungumza jana, katika soko la Bunazi lililopo Wilaya ya Misenyi, Dk Kasangala alisema kampeni ya mtu kwa mtu anayoifanya ina ushawishi mkubwa kwa vile inamfikia hata asiyehudhuria mikutano ya kampeni za kudhibiti ebola inayofanywa kuanzia ngazi za chini za mitaa na vijiji.
“Tutaendelea na kasi hii, tutashambulia kila mahali, nyumba za wageni chumba kwa chumba, wageni wanaingia na kutoka wapate elimu ya kujikinga na ebola na tutashambulia mitaani na tutashambulia nyumba hadi nyumba na mtu hadi mtu, hakuna kulala, serikali haitalala hadi hapo nchi jirani itakapotuhakikishia wameudhibiti ugoñjwa huu,” alisema.
Alisema tayari wametoa maagizo kwenye nyumba zote za wageni kuzingatia afua za afya kwa kuweka sabuni, maji tiririka na kuwapima joto wageni wote wanaoingia.
“Tumewaelimisha na kama kuna mgeni muhisiwa basi wapige simu namba 199 ni bure na kutoa taarifa na wataalamu wetu watachukua hatua kwa haraka.
Alisema mbali na kutembea nyumba hadi nyumba, bado wataendelea kutumia magari ya matangazo kuzunguka kwenye maeneo ya pembezoñi kuelimisha wananchi.
Aidha, kātika kampeni hizo, Dk Kasangala aligawa vipeperushi vyenye ujumbe kuhusu dalili za ugonjwa wa Ebola na namna ya kujikinga
Katika soko la Bunazi lililopo wilayani Misenyi, Dk Kasangala aligawa vizibao vyenye ujumbe wa kujikinga na Ebola kwa madereva wa bodaboda, aligawa vipeperushi kwa wafanyabiashara mbalimbali na wananchi waliofika kununua mahitaji ikiwemo flashi ambazo zinazungumzia ugonjwa huo wa Ebola.
Dk Kasangala alisema serikali imeweka nguvu kubwa mkoani Kagera kutokana na mkoa huo kuingiliana kwa karibu na Uganda.