Eneo la uongezeaji thamani madini mbioni

KAHAMA: Serikali imedhamiria kutekeleza  sera ya uongezaji thamani ya madini ndani ya nchi kwa kutengeneza bidhaa zitokanazo na madini ghafi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika uzinduzi Kituo cha Barick – Buzwagi ambacho kitakwenda kutoa mafunzo mbalimbali  katika kuongeza uelewa na maarifa katika masuala muhimu ya kwenye sekta ya madini.

Amesema, serikali inatarajia kutenga eneo maalumu la ukanda wa kiuchumi (Buzwagi Special Economic Zone) katika eneo la ekari 1333 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini na uzalishaji wa bidhaa za migodini ambapo awali palikuwa pakifanyika shughuli za uchimbaji madini kupitia Kampuni ya madini ya Barrick.

Aidha,  Mavunde amesema  moja kati ya maelekezo ya Rais  Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha madini  yanaongezewa thamani nchini na kuongeza fursa za ajira kwa watanzania,kuongeza ujuzi kwa nguvu kazi na kuchochea upatikanaji wa mapato ya nchi.

“Na hapa Buzwagi ndio panakwenda kuleta mabadiliko makubwa, muitikio wa ujenzi wa viwanda katika eneo hili umekuwa mkubwa na hasa katika viwanda vya kuongeza thamani madini na uzalishaji wa bidhaa za migodini ambazo awali nyingi zilikuwa zinanunuliwa nje ya nchi na sasa kupitia viwanda hivi zitapatikana hapa nchini, “amesema Mavunde

Amesema, viwanda vitakavyokuwepo kwa awamu ya kwanza Kiwanda cha usafishaji na uongezaji madini thamani  ambacho kipo  chini ya Kampuni ya  Tembo Nickel.

Awali Mkuu wa Wilaya wa Kahama Mboni Mhita ameipongeza na kuishurkuru Kampuni ya Barick kwa uwekezaji wa kipekee katika eneo la Kahama pamoja na ushirikiano mzuri baina ya Serikali na Kampuni ya Barick na kusema kwamba hatua hizo za makusudi zitasaidia kuchochea uchumi wa wilaya ya Kahama ambao baada ya mgodi wa Buzwagi kufungwa ulidorora.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Barick Dk Mark Bristow  ameeleza kuwa Kampuni yao  inaunga mkono juhudi za Serikali  Juu ya uongezaji thamani madini na ushiriki wa wazawa kwa kuwekeza kwenye elimu ya vijana kama vile kituo cha mafunzo kwa wadau wa madini cha ‘Barick Academy’  ambacho kinatarajiwa kutoa mafunzo kwa watu 1024 kwa mwaka 2024, akaongeza pia wapo mbioni kuwapa nafasi za juu za uendeshaji migodi hapa nchini hiyo kwa watanzania.

Naye Mbunge wa Kahama Mjini Jumanne Kishimba ameiomba Kampuni ya Barrick kuandaa mafunzo mafupi kwa wachimbaji wadogo kuwafundisha usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini na hasa dhahabu kwa kuwa wananchi wengi ambao ni wachimbaji hawana uelewa mkubwa wa biashara ya madini.

Habari Zifananazo

Back to top button