Epukeni kujiingiza kwenye makosa ya kimtandao

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetoa taarifa juu ya kumkamata mtuhumiwa mmoja kwa tuhuma za makosa ya kimtandao. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro mtuhumiwa huyo alifahamika kwa jina la Innocent Chuwa ambaye ni mkazi wa Kijichi, Temeke.

Jeshi hilo lilisema uchunguzi utakapokamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa katika mikono ya sheria. Machi 7, 2025, jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 25 kwa tuhuma za makosa kama hayo ya kimtandao, katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine ya jirani.

Inadaiwa kuwa, mara nyingi watu hao hujihusisha na vitendo vya kutumia laini za simu zisizo na usajili wao na kutuma jumbe zinazomtaka mtu kutuma kiasi cha fedha kama vile kodi, ada au fedha za matibabu ya mtoto wake. SOMA: ‘Demokrasia haijengwi kwa kuvuruga amani’

Nafikiri sio mgeni wa ujumbe kama vile ‘ile hela tuma kwenye namba hii’ kwenye simu yako. Watu hao hutumia njia nyingine ya kuingilia na kubadili namba za utambuzi halisi wa simu. Kadhalika, wengine hutumia mitandao ya kijamii kudhalilisha watu kwa kutumia programu za akili mnemba, ambazo hutumia sura ya mtu mwingine kuweka maneno au vitendo tofauti yanayoashiria kudhalilisha na kutweza utu wa mtu.

Nafikiri ni wakati Watanzania kufahamu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, kwani mitandao ya kijamii sasa hivi ni eneo linaloweza kukuunganisha na fursa nyingi zilizopo ulimwenguni. Mitandao ya kijamii imekuwa ni njia ya kupata masoko, kupata bidhaa na kuunganishwa na watu. Hivyo, katika eneo la biashara, ni vyema watu wakabadili mitazamo yao na kuiangalia katika mtazamo chanya na kuzitumia fursa tele zilizopo kwenye mitandao Sambamba na hilo, Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa hakuna uhuru usio na mipaka.

Hata katika kujipatia fursa hizo, ni wazi kuwa tunapaswa kufahamu kuwa nchi hii inaendeshwa na sheria, ikiwemo Sheria ya Makosa ya Mitandao ya 2015, ambayo inaweza kumuweka mtu hatiani kwa makosa ya kimtandao na kuwajibishwa vilevile Ni aibu kuona mpaka sasa kuna watu wanatuma jumbe zenye nia ya kuwatapeli watu, badala ya kutumia mtandao kujipatia kipato cha halali. Kwa kuzingatia kwamba jeshi la polisi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanaendelea kupambana na wahalifu hawa wa kimtandao, tunawapongeza na kuwasihi waendelee kukaza buti kushughulika nao ili kumaliza kabisa tatizo la uhalifu wa kimtandao.

Nafikiri vyombo hivi pia vina wajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya uwepo wa sheria na wajue kuwa sheria hizo zinafanya kazi na kuwa serikali haijalala, ipo macho inawaangalia.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button