ETDCO wakamilisha kilovolti 132 Tabora – Katavi

KATAVI: KAMPUNI ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekamilisha ujenzi wa laini mpya ya umeme yenye msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Katavi.
Laini hiyo yenye urefu wa kilometa 383, kukamilika kwake ni hatua muhimu ya kuunganisha Mkoa wa Katavi na Gridi ya Taifa.
Akizungumza wakati wa majaribio ya laini hiyo katika kituo cha kupoza umeme cha Mpanda mkoani Katavi, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Sadock Mugendi, alisema ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 100.
Mugendi aliishukuru serikali na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kuiamini kampuni hiyo kutekeleza mradi huo wa kimkakati.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO,Dismas Massawe, alisema gharama ya mradi huo ni shilingi bilioni 116, fedha ambazo zimetolewa na serikali.
Alisema gharama hiyo inahusisha ujenzi wa laini ya kusafirisha umeme kwa umbali wa kilometa 383 kutoka Tabora hadi Mpanda-Katavi.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali za kupeleka umeme wa uhakika wa Gridi ya Taifa kwenye maeneo ambayo hayakuwa yameunganishwa awali, kama Mkoa wa Katavi ikiwa na lengo la kuchochea maendeleo kwa kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira.