Ewura yapiga marufuku kukata maji wikiendi

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imesema ni marufuku kwa mamlaka za maji nchini kukata maji mwishoni mwa wiki kwa sababu kufanya hivyo ni kama unyanyasaji.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa EWURA, Titus Kaguo kwenye semina kwa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya habari nchini (JOWUTA).

Amesema kitendo cha mtu kukatiwa maji kuanzia Ijumaa saa 12 jioni au Jumamosi na Jumapili hairuhusiwi kiutaratibu na kiudhibiti.

Advertisement

“Mtu anayefanya hivyo asifanye tena kwasababu anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria ili kuwajibika kwa kile anachokifanya,”amesema.

Amesema Watanzania wajenge utamaduni wa kusoma mikataba ya huduma kwa wateja kwani inawapa wajibu wa wao wafanye nini na mamlaka zifanye nini.

Kaguo amesema mamlaka zimekuwa hazihamasishi mikataba hiyo ili Watanzania wasiibuke na kuanza kudai haki zao.
Pia, amesema kuwa wakati wa usomaji wa mita za maji, ofisa wa mamlaka ya maji hapaswi kuisoma akiwa mwenyewe na badala yake anatakiwa kusubiri wenye nyumba.

Amesema hali hiyo imekuwa ikileta malalamiko mbalimbali kuhusu kubambikiwa bili za maji kutokana na kutohusika wakati wa usomaji wa mita.

‘’Ni lazima awepo mtu wakati wa kusoma mita za maji na baada ya kusoma mteja atumiwe ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya simu na baada ya siku tatu ndio atumiwe bili,’’ amesema.

Alifafanua kuwa sababu za kutoa siku tatu kabla ya kutuma bili ni kutoa nafasi kwa wateja kama wanaridhika na taarifa waliyopata au kama wana malalamiko waweze kuyawasilisha kabla ya kutumiwa bili.

Kaguo amesema si sahihi kwa wafanyakazi wa mamlaka hizo kutuma bili za miezi ya nyuma ikiwa mteja ameshalipa bili za mbele.

Kadhalika, amesema wateja wa maji wana haki ya kupata taarifa kuhusu huduma za maji zinazotolewa na mamlaka husika ikiwemo ukataji wa maji kutokana na hitilafu mbalimbali.

Katibu Mkuu wa Jowuta Seleman Msuya amesema elimu waliyotoa Ewura inawafanya waandishi wa habari kwenda kuwa mabalozi wa kutoa habari sahihi zinazohusiana na Ewura na kuwasaidia wananchi.

Ameomba Ewura kuendelea kuwafikia wanachama wa Jowuta wa mikoani ili na wao waweze kunufaika na hatimaye washiriki kikamilifu kuelimisha wananchi mambo mbalimbali yanayohusu mikataba.