Faru weusi kuongeza watalii Mkomazi

KILIMANJARO: Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi imeendelea kuibuka kuwa moja ya vivutio muhimu vya utalii nchini Tanzania, huku utalii wa faru weusi ukitajwa kuwa kivutio kikubwa kinachoongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.

Hifadhi hiyo, iliyopo katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, ina ukubwa wa kilometa za mraba 3,245 na iko takribani kilometa 112 kutoka Moshi mjini.

Mkomazi ilitangazwa rasmi kuwa Hifadhi ya Taifa mwaka 2008 na sasa ni miongoni mwa hifadhi 21 zinazosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Utalii wa Faru Weusi ulianzishwa mwaka 2021 ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza idadi na kulinda faru ambao ni miongoni mwa wanyama walio katika hatari ya kutoweka.

Tangu kuanzishwa kwa utalii huo, idadi ya watalii wanaotembelea Mkomazi imeongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka takribani watalii 1,000 mwaka 2021 hadi kufikia 10,000 kwa mwaka kwa sasa.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Eva Mallya, amesema utalii wa Faru Weusi umekuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vinavyowavutia watalii katika hifadhi hiyo.

“Njoo Hifadhi ya Mkomazi, utakuwa na uhakika wa asilimia 99 kumuona faru,” amesema Mallya, akieleza kuwa watalii wanaweza kupata fursa ya kuwaona wanyama hao katika mazingira yao ya asili.

Miongoni mwa vivutio vinavyozidi kupata umaarufu ni Faru Kisima, faru yatima ambaye mama yake alifariki akiwa bado mdogo.

Kupitia utalii wa faru, wageni pia wanaweza kushiriki katika mpango wa kuasili faru, hususan faru yatima kama Kisima, ambapo mgeni anaweza kuchangia gharama zinazohitajika kwa ajili ya maisha na ustawi wa faru huyo.

Mbali na faru, Mkomazi ina wanyamapori mbalimbali wakiwemo swala, twiga, tembo, simba, chui na nyati, ambao watalii wanaweza kuwaona wakati wa safari za utalii ndani ya hifadhi.

Mkomazi pia inatoa aina mbalimbali za utalii, zikiwemo utalii wa mchana, utalii wa usiku na utalii wa kutembea kwa miguu, hivyo kumpa mgeni fursa ya kuchagua aina ya safari inayomfaa.

Kwa upande wa miundombinu, uwepo wa viwanja viwili vya ndege vya Kisima na Mkomazi, vilivyojengwa kwa fedha zilizotengwa wakati wa UVIKO-19, umeendelea kurahisisha upatikanaji wa hifadhi hiyo kwa watalii.

Kutoka Tanga mjini, mgeni anahitaji kusafiri takribani kilometa 100 kufika Mkomazi, ambapo sehemu ya barabara ni ya lami na sehemu nyingine ni moramu iliyoboreshwa kwa kiwango kinachowezesha kupitika wakati wote.

Filamu za The Royal Tour na Amazing Tanzania pia zimetajwa kuwa na mchango katika kuitangaza Tanzania na vivutio vyake, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Mallya amesema filamu hizo, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zimekuwa kichocheo muhimu katika kuitangaza sekta ya utalii nchini na kuwafikia watalii wa ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, amesema kuanzishwa kwa Same Utalii Festival wilayani Same kumeongeza mwamko wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika eneo hilo, ikiwemo Mkomazi.

Akizungumza kuhusu ziara ya waandishi wa habari katika hifadhi hiyo, Mallya aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwezesha ziara hiyo.

“Nichukue fursa hii kumpongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, kwa kutuletea timu hii ya waandishi wa habari katika Hifadhi ya Mkomazi. Tunaamini kupitia kwenu Mkomazi inakwenda kuitangaza Mkomazi kitaifa na kimataifa,” amesema Mallya.

Kwa kuendelea kuimarisha miundombinu, kutangaza vivutio na kukuza utalii wa faru, Mkomazi inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuendelea kuongeza idadi ya watalii na kuchangia katika uhifadhi wa wanyamapori pamoja na uchumi wa taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button