FCC yatakiwa kudhibiti bidhaa feki

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameihimiza Tume ya Ushindani (FCC) kuongeza ufanisi katika kudhibiti bidhaa feki na kuimarisha utendaji ili kukidhi matarajio ya Watanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam alipotembelea makao makuu ya tume hiyo, Waziri Kapinga amesema ni muhimu FCC kuwa na mifumo thabiti ya ufuatiliaji na usimamizi wa bidhaa zinazoingia sokoni.
Amesema sekta ya biashara ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuongeza ushindani na kupanua mapato ya nje ya nchi, hivyo juhudi za kukomesha bidhaa feki zinapaswa kupewa kipaumbele ili kulinda maslahi ya wananchi na uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, ameahidi kutekeleza maelekezo ya serikali na kuboresha mifumo ya usimamizi wa bidhaa zinazoingizwa nchini. Amesema kuanzia Desemba 1, FCC itaanza kurekodi taarifa za wasafirishaji wa bidhaa zote ili kurahisisha ukaguzi na udhibiti wa bidhaa zisizokidhi viwango.
FCC imeahidi kuendelea kushirikiana na sekta binafsi na mamlaka husika ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia sokoni ni salama, zenye ubora na zinazingatia viwango vya kitaifa. SOMA: Takukuru yabaini risiti feki za EFD Shinyanga



