FETA yatakiwa kutanua wigo wa mashirikiano katika kutoa mafunzo

Feta yatakiwa kutanua wigo wa mashirikiano katika kutoa mafunzo

Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) imetakiwa kuongeza wigo wa mashirikiano katika kutoe elimu ya uvuvi.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Mohamed Shekh wakati akifunga mafunzo ya siku 30 ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa mazao ya samaki juu ya usalama, ubora na taratibu za ukaguzi kutoka nchini Somali.

Profesa Shekh amesema kuwa FETA inatakiwa kuongeza wigo wa mashirikiano na nchi mbalimbali kwani zipo rasilimali nyingi na wataalam wapo wa kutosha hivyo haitakiwi wataalam kujifungia wenyewe bali wajitokeze.

Advertisement

Vilevile amewasihi kuendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo kwa watu wa ndani na nje ya nchi hasa wanaijishughulisha na shughuli za uvuvi.

Alisema Wataalam wa uvuvi kutoka Somalia wamekuwa wakishiriki mafunzo hayo hapa nchini kwa lengo la kuongeza uwezo katika kusimamia rasilimali za uvuvi na kuhakikisha kuwa kuna kuwa na uvuvi endelevu nchini kwao.

Profesa Shekh amesema upo umuhimu mkubwa katika kuhakikisha mazao ya bahari yanakuwa na ubora unaotakiwa, hivyo ameitaka FETA kuhakikisha inaendela kuhamasisha na kutoa mafunzo hayo kwa washiriki kutoka nchi mbalimbali.

Vilevile amelishukuru Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo ambapo ameyaomba na mashirika mengine kuiga mfano huo ili kuwezesha mafunzo hayo kuwafikia washiriki wengi zaidi.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dk Semvua Mzighani amesema kuwa mafunzo yanayotolewa chuoni hapo msisitizo mkubwa huwa ni kwenye kufanya mafunzo kwa vitendo.

Amesema  ni matarajio yake kuwa watakaporejea nchini kwao watakwenda kutekeleza yale waliyofundishwa kwa vitendo kitu ambacho kitawaongezea ujuzi zaidi na kusaidia kutoa elimu kwa wengine.

Akiongea kwa niaba ya wanafunzi wengine Rais wa wanafunzi hao kutoka chuo cha Uvuvi nchini Somalia  Elm Mohamed alisema kuwa ni vyema  nchi  zikashirikiana katika rasilimali  kwani zinafanana hasa ukanda wa bahari pamoja na ufugaji .

Mafunzo hayo ya mwezi mmoja yameanza tarehe 12/05/2023 na kumalizika tarehe 13/06/2023 ambapo pamoja na mafunzo washiriki wamepata fursa ya kujifunza Kiswahili na Tamaduni za Kitanzania.

mafunzo yameyofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Chuo cha Mafunzo ya Uvuvi Kampasi ya Mbegani wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.