Fifa yazifungia klabu tano kusajili

Clifford Ndimbo

DAR ES SALAAM – KLABU tano zimefungiwa kusajili na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) hadi watakapowalipa wachezaji wanaowadai.

Akizungumza na HabariLEO, Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alitaja klabu zilizofungiwa ni Yanga, Tabora United, Singida Fountain Gate FC, Biashara United na FGA Talent FC.

Yanga iliyofungiwa Aprili mwaka huu kusajili kutokana na kutokamilisha usajili wa mchezaji wake kwenye mfumo wa Fifa, bado inadaiwa na mchezaji Lazarous Kambole.

Advertisement

Tabora United imekuwa na mwendelezo wa kufungiwa mara kwa mara na mara ya mwisho Mei 8, mwaka huu ilifungiwa hadi itakapomlipa Makuntima Kisombe raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Singida Fountain Gate FC ilifungiwa kusajili hadi itakapomlipa ada ya uhamisho na malimbikizo ya mishahara mchezaji raia wa Uganda, Shafik Batambuzi.

SOMA: Ntibazonkiza Ntibazonkiza yametimia Simba

FGA Talent ilifungiwa kwa kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu na aliyewahi kuwa kocha wao Ahmed El Fatamany pamoja na Tabora United. Taarifa ya TFF imebainisha kuwa wachezaji hao walifungua kesi Fifa wakidai malipo ya malimbikizo ya mishahara na fidia ya kuvunjiwa mkataba dhidi ya klabu hizo.

“TFF inazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.

“Klabu ambayo itawalipa wahusika, itaondolewa mara moja adhabu ya kufungiwa kusajili hadi leo asubuhi kupitia mfumo wa Fifa (FIFA Legal portal) hakuna taarifa ya klabu yoyote kati ya hizo iliyowalipa wahusika,” aliongeza Ndimbo.