Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Bodi ya Filamu Tanzania na Michezo ya Kuigiza imeandaa Mkakati madhubuti wa kuandaa filamu tano zitakazoelezea utamaduni, vivutio vya ndani, historia na kuhamasisha uzalendo na utaifa kwa vizazi vijavyo.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro amesema hayo leo Oktoba 23, Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kuhusu mikakati madhubuti ya kukuza Sanaa nchini hususani tasnia ya Filamu, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Mwenyekiti wake, Husna Sekiboko.
SOMA: Filamu za Tanzania zachomoza Netflix
Ndumbaro amezitaja Filamu hizo kuwa ni Filamu ya Chifu Kingalu, Filamu ya Asante, Filamu ya Mwalimu Nyerere, Tamthilia inayohusu masuala ya Bima na Filamu ya A Trip With Your Wife, lengo likiwa ni kuitangaza Tanzania katika nyanja mbalimbali kupitia filamu na kuwatafutia soko wadau wa filamu nje ya Tanzania.
“Kwa sasa Bodi inakamilisha Mkakati wa kuunganisha Mfumo wa kidigiti wa (Arts Management Information System – AMIS) na mifumo mingine ya TAUSI kutoka TAMISEMI, COSOTA NIDA, BRELA na TRA ili kuwafikia wadau bila kufika ofisi za Bodi kupata huduma,” amesema Ndumbaro.
Wakichangia taarifa hiyo, Wajumbe wa Kamati wameelekeza wizara kupitia Bodi ya Filamu, kutengeneza mpango mahususi wa kuunga mkono uandaaji na usambazaji wa Filamu za Tanzania pamoja na kuwafikia wasanii walioko vijijini.