Fistula yazua mjadala mpya

MBEYA : WATOA Huduma za Afya ya mama na mtoto wametakiwa kuwa makini wakati wa kutoa huduma za uzazi ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kwa mama mjamzito, ikiwemo ugonjwa wa fistula unaowaathiri wanawake wengi hasa kutoka maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma bora za afya.
Rai hiyo imetolewa Mei 21, 2025, jijini Mbeya na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwaji, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau kujadili afua muhimu za kupambana na ugonjwa wa fistula.
Dkt. Mbwaji amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika huduma za afya ya mama na mtoto, hivyo ni jukumu la watoa huduma kuhakikisha kila mama anajifungua salama na bila kupata matatizo ya kiafya kama vile fistula.
“Mama anapojifungua hatakiwi kubaki na tatizo lolote la kiafya. Ni jukumu letu kumlinda mama huyu wa thamani dhidi ya ugonjwa wa fistula kwa ajili ya uzazi endelevu na maendeleo ya Taifa,” amesema Dkt. Mbwaji.
Kwa upande wake, Mratibu wa Afua za Fistula Tanzania, Fidea Obimbo, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa huduma muhimu za kupambana na fistula kwa kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa kupitia madaktari wa Dkt. Samia Mobile Clinic.
Ameongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Kitengo cha Mama na Mtoto, yakilenga kutoa huduma za upasuaji na elimu kuhusu ugonjwa huo kwa jamii.
“Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali wa afya kujitokeza na kushiriki kikamilifu kwa kuchangia huduma, elimu na rasilimali kwa ajili ya kupambana na fistula. Changamoto kubwa ni kuwa idadi ya watoa huduma bado ni ndogo sana,” amesema Fidea.
Naye Mkurugenzi wa Fistula Foundation, Clement Ndahani, amesema ugonjwa wa fistula huathiri zaidi wanawake wanaotoka katika kaya masikini, huku wengi wao wakikosa uelewa wa kutosha kuhusu tiba ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dkt. Rebeca Mokeha, amesema Mkoa wa Mbeya unakadiriwa kuwa na zaidi ya wanawake 3,000 wenye tatizo la fistula, lakini ni wanawake 1,000 pekee wanaofanyiwa upasuaji kila mwaka kutokana na changamoto ya uhamasishaji na imani potofu.
“Wapo wanaoamini kuwa fistula ni laana au ugonjwa usiotibika. Hii ni dhana potofu. Tunahitaji elimu ya kutosha katika jamii ili kuokoa maisha ya wanawake hawa,” amesema Dkt. Mokeha.
Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Fistula Duniani hufanyika Mei 23 kila mwaka. Kwa mwaka huu, yanaadhimishwa mkoani Mbeya yakiwa na kauli mbiu isemayo: “Afya ni Haki ya Kila Mwanamke, Tengeneza Hatma Yake, Pasipo Fistula.”



