Serikali yaandaa mpango kutokomeza ugonjwa fistula

SERIKALI imetangaza azma ya kutekeleza kwa vitendo mpango wa kuondoa tatizo la ugonjwa wa fi stula kwa wanawake wakati wa kujifungua.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitangaza hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Fistula ambayo kitaifa yamefanyika wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kwamba mpango huo unalenga kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Profesa Pascal Rugajo kwa niaba ya Ummy alisema moja ya mipango mikakati katika kutekeleza hilo ni uwepo wa vituo vya kutoa huduma za uzazi salama. Rugajo alisema hadi sasa huduma hizo zinatolewa kwenye vituo 503 nchini kwenye vituo vya afya na zahanati.

Advertisement

“Kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wa fistula 21,400 kutoka idadi ya wagonjwa 50,000 waliopo duniani hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha wagonjwa hao wanafikiwa na kupata matibabu,” alisema mkurugenzi huyo wa tiba.

Profesa Rugajo alisema serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa huduma kwa waathirika na kuongeza utoaji huduma ili ziweze kutolewa nchi nzima kuwezesha kurudisha tabasamu kwa wanawake waliopatwa na tatizo hilo.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Americares, Dk Nguke Mwakatundu alisema changamoto ya fistula nchini bado ni kubwa, hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau hawana budi kufanya kazi kwa pamoja na kuongeza juhudi kukabiliana na tatizo hilo.

Dk Mwakatundu alisema tangu mwaka 2011 shirika hilo lianze kutoa huduma za afya limewezesha kupatiwa matibabu kwa wagonjwa 2,000 katika Hospitali ya Bugando na kubainisha kuwa kila mwaka wagonjwa wapya 2,500 wanatokea nchini huku 1,500 wakipata matibabu.

Alisema ni lazima huduma za uzazi salama ziimarishwe sambamba na kusogezwa karibu kwa huduma za upasuaji kwa waathirika wa ugonjwa wa fistula. Meneja Miradi wa Shirika la CCBRT, Yohana Kaswalala alisema takwimu zinaonesha kuna wanawake zaidi ya 500,000 Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao wana matatizo ya fistula na kati yao, 10,000 wakiwa nchini Tanzania.