“Fuateni sheria kuepuka misuguano”

DAR ES SALAAM: NAIBU msajili wa vyama vya siasa nchini, Sisty Nyahoza amevitaka vyama vya siasa kuzingatia sheria zilizowekwa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili kudumisha amani na uzalendo.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK) wa kuchagua wagombea jijini Dar es Salaam amesema uwepo wa amani ndani ya nchi ndio unaofanikisha shughuli za siasa kufanikiwa.
“Hata hapa tulipo umoja wetu ndio unatufanya tuwe pamoja hapa tukiwa wazanzibari na watu wa bara hivyo tulinde umoja wetu ili tufanye siasa kwa amani na utuliva,”amesisitiza.
Nyahoza amesema mkutano huo umefanyika kwa sababu taifa lina amani na hivyo mtu yeyote mwenye nia ya kuvunja amani ni vyema akakemewa mapema.

Aidha, amekipongeza chama hicho kwa kufanya uchaguzi wa wazi na demokrasia wa kumchagua Mgombea Urais wa Tanzania Bara na Zanzibar kupitia chama hicho.
Amesema chama hicho kimekidhi vigezo kwa kuwa na wajumbe wa mkutano mkuu 87 kwa mujibu wa sheria hivyo mkutano wao umekwenda vizuri.
Katika uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Chama hicho, David Mwaijojele ameibuka mshindi mgombea kiti cha Urais kwa Tanzania Bara huku Isha Salum akiteuliwa na Halmashauri Kuu kuwa mgombea pekee wa nafasi ya urais kwa upande wa Zanzibar.

Akizungumza baada ya kushinda Mwaijojele amesema kuwa malengo yao ni kutaka kuhakikisha jamii ya kitanzania inaishi maisha bora katika maeneo mbalimbali ya kilimo, uvuvi, ujasiriamali ikiwemo makundi maalumu.
‘Chama cha CCM tutakapopewa ridhaa kupitia tume tutahakikisha vijana wanaweza kujiajiri wenyewe pindi wanapomaliza elimu,lakini pia wanawake kunufaika na uchumi wao,”amesema Mwaijolele.

Naye Aisha Hamadi amesema kuwa yupo tayari kukipambania chama cha CCK kwa Zanzibar ambapo vipaumbele vyake ni kuwasaidia watu wenye uhitaji ikiwemo walemavu.
“Watanzani watuunge mkono kwa kukichagua chama hiki ili kiweze kuwasaidi kutatua changamoto mbalimbali kwenye maeneo yao.



