Fursa za uvuvi, utalii wa bahari kuibuliwa COP12

DAR ES SALAAM: FURSA za uwekezaji katika sekta ya uvuvi, ufugaji wa samaki, usindikaji wa mazao ya baharini, utalii wa bahari, usafirishaji wa majini, bandari, mafuta na gesi zimepewa kipaumbele kupitia Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amesema COP12 inalenga kuibua miradi na programu za pamoja zitakazochochea uwekezaji katika uchumi wa buluu huku zikihakikisha uhifadhi wa mazingira ya Bahari ya Hindi.
Amesema fursa hizo zina uwezo wa kuongeza ajira na kipato kwa wananchi pamoja na mapato ya Serikali endapo zitatumika kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, akitoa mfano wa utalii wa bahari ambao unaweza kuongeza idadi ya watalii na manufaa ya kiuchumi.
Masauni amesema ushiriki wa washirika wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali umefungua fursa ya kutafuta rasilimali za kuwezesha utekelezaji wa miradi ya pamoja ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, akisisitiza kuwa Tanzania inalenga kuhakikisha mkutano huo unazalisha miradi, programu na mikakati inayotekelezeka badala ya kuishia katika mijadala na maazimio.
Amesema kwa kuwa Tanzania na nchi nyingine zinazopakana na Bahari ya Hindi zinakabiliwa na changamoto zinazofanana, kuna umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kuandaa mipango itakayolinda mazingira na kuongeza manufaa ya kiuchumi yatokanayo na bahari. Pia alisema zaidi ya washiriki 700 kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo wadau wa maendeleo, mazingira na sekta mbalimbali za uchumi, wanashiriki mkutano huo.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya COP12, Tanzania imeandaa vikao maalumu kwa wanawake na vijana kwa lengo la kuwaongezea nafasi ya kushiriki katika shughuli za uchumi wa buluu, ubunifu na matumizi ya teknolojia. Masauni alisema jukwaa la wanawake linatoa fursa ya kujenga ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuanzisha mahusiano ya kibiashara, huku akisisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa buluu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Muungano na Mazingira) Zanzibar, Khamis Juma Khamis, amesema mshikamano wa nchi wanachama ni muhimu katika kukabiliana na uchafuzi wa bahari na uharibifu wa matumbawe unaotishia mazalia ya samaki na maisha ya jamii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Dk Elizabeth Mrema, amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi wa bahari, akisema uchafu wa plastiki ni miongoni mwa vitisho vinavyoathiri viumbe vya baharini na jamii zinazotegemea rasilimali hizo.



