NAIROBI, Kenya: NAIBU Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua ameendelea kujitetea tangu jana na tena leo anaendelea na utetezi wake bungeni kwa kujenga hoja zinazochagizwa na ushahidi wa video.
Gachagua anatuhumiwa kwa makosa 11 ikiwemo, ufisadi, ukiukwaji wa katiba, kutomheshimu Rais na Mawaziri, kuendeleza ukabila.
“Madai dhidi yangu hayana msingi,” amejitetea naibu huyo.
Hoja za kumtia hatiani Gachagua ziliwasilishwa bungeni na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Bwengi Mutuse.
Katika maelezo yake, Mutuse anamtuhumu, Gachagua kwa ukiukaji wa kipengele cha 10, 27, 73, 75 na 129 cha Katiba ya sasa kwa kueneza ukabila, ubaguzi na kusababisha migawanyiko kitaifa.
“Kwa mfano wakati mmoja mnamo 2023 katika mkutano wa hadhara katika kaunti ya Kajiado, Naibu Rais alitoa matamshi ya kuchochezi kwamba Serikali ya Kenya ni Kampuni na kwamba ugavi wa miradi ya maendeleo na rasilimali ya umma inapasa kufanywa kwa misingi ya ‘hisa’ inayokadiriwa kutokana na jinsi watu kutoka jamii mbalimbali walipiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2022. Kauli kama hii inaendeleza ukabila, ubaguzi na kuvunja utaifa,” amedadavua ndani ya hoja yake.
Wabunge 291 wameunga mkono hoja hizo, hata hivyo, Spika wa Bunge la kitaifa, Moses Wetangula amekosoa hatua ya Gachagua kufanya mkutano na waandishi wa habari Oktoba 8, kitendo alichokiita kuwa ni cha kusikitisha.
Taratibu za bunge zimejipambanua kuwa iwapo theluthi mbili (233) ya wabunge 349 itaunga mkono Gachagua kung’oka, hoja hiyo itawasilishwa kwa Seneti.
Hata hivyo ikiwa wabunge 117 wataikataa, Naibu wa Rais atasalia madarakani.