Gari ya umeme UDSM kupunguza gharama za mafuta

GARI inayotumia umeme imetengenezwa kwa lengo la kupunguza gharama kubwa zinazotokana na utumiaji wa mafuta ya petroli au dizeli.

Hayo yameelezwa na Aston Nyenyembe kutoka Ndaki ya Uhandisi katika kitengo cha ubunifu na uendelezaji wa teknolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika maadhimisho ya nane ya wiki ya utafiti na ubunifu chuoni hapo.

Akizungumzia gari hilo Nyenyembe amesema gari hiyo inachajiwa saa tatu au nne kwenye umeme, baada ya hapo inaweza kutembea kilomita 100 hadi 120.

Amesema wapo tayari kuuza teknolojia hiyo kwa mwekezaji yeyote atakayehitaji, lakini pia wanamkaribisha mwekezaji atakayeweza kuwasimamia kama chuo ili watengeneze magari.

Ametaja gharama ya gari hilo kuwa itaongezwa milioni mbili au tatu juu ya gharama ya kununulia bajaji.

“Mpaka sasa wapo wadau na wateja walioonesha nia ya kununua teknolojia au gari hiyo zikiwemo hoteli, viwanja vya mpira, migodini na wengineo,” amesema.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema chuo hicho kinaunga mkono jitihada za serikali za kuhamasisha tafiti kama njia ya kutafuta suluhu ya matatizo ya jamii ya watanzania.

” Mwaka 2012 chuo kilizindua dira ya mwaka 2061 inayolenga kukifanya chuo kikuu kuendelea kuwa kituo cha maarifa na ubunifu kwa maendeleo endelevu ya Tanzania na Afrika kwa ujumla,” amesema.

Amesema dira hiyo inaainisha uhamasishaji wa walimu na wanafunzi katika ujifunzaji na ufundishaji, utafiti na ubadilishanaji maarifa.

Pia uongozi wenye maono na dira ya kufikisha malengo yanayokusudiwa pia uongozi wa kimkakati, usawa wa kijinsia na kudhibiti ubora katika elimu.

Habari Zifananazo

Back to top button