Gavana BoT atoa maelekezo maduka fedha za kigeni

ARUSHA: BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wamiliki wa hoteli za nyota tatu hadi tano nchini kuhakikisha hadi ifikapo Julai Mosi, mwaka huu wawe wameshakata leseni ya kumiliki na kuendesha maduka ya
kubadilishia fedha za kigeni kwenye hoteli zao.

Hayo yamebainishwa na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba wakati wa kikao maalumu na wamiliki wa hoteli jijini Arusha jana kwa lengo la kupokea maoni yao kuhusu maduka hayo.

Tutuba amesema sekta ya hoteli ni wadau muhimu kwa uchumi wa nchi kwa kuwa ni sekta iliyoungana na sekta ya utalii kwa kuwapokea, kuwahifadhi na kuwahudumia watalii.

Advertisement

Amesema kwa kuwa baadhi ya watalii hufika kwenye hoteli hizo nyakati za usiku au nyakati za sikukuu hali inayowafanya washindwe kupata huduma ya kubadilisha fedha za kigeni walizonazo, hivyo amesema BoT imeamua kubadilisha kanuni zake kwa kuruhusu wamiliki wa hoteli hizo kuwa na maduka ya kubadilishia fedha za kigeni kwa ajili ya wageni wanaowapokea.

Kwa mujibu wa Tutuba, baadhi ya hoteli hutoa huduma hiyo ya kubadilisha fedha za kigeni kinyemela jambo ambalo ni kosa kisheria kwa kuwa soko hilo ni haramu na kwa kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi.

Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa hoteli walionesha hofu ya usalama wao kumiliki maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kwenye hoteli zao jambo ambalo Tutuba amewaondolea hofu kwa kuwaambia kuwa utawekwa utaratibu mzuri ikiwemo kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wao.

Mmoja wa wamiliki hao wa hoteli, Wilbard Chambulo amesema anamiliki hoteli takribani 33, hivyo ni vyema BoT ikahama kutoka kwenye mfumo wa kutumia fedha taslimu iwe fedha za kigeni au shilingi badala yake waimarishe mifumo kielektroniki kwa matumizi ya kadi ambayo ni salama na unaingiza mapato halali kwa wamiliki wa hoteli na serikali.

Chambulo pia amemweleza Gavana kuwa wamiliki wa hoteli hawahusiki na masoko haramu ya kubadilishia fedha za kigeni au kutoza fedha za kigeni hususani dola kwenye huduma zao bali afanye uchunguzi na atabaini wahusika.