Makubaliano kuimarisha sekta binafsi

UFARANSA: Tanzania Private Sector Federation (TPSF) na International Chamber of Commerce (ICC) leo wameingia makubaliano ya kimkakati yatakayopanua ushirikiano kati ya sekta binafsi ya Tanzania na jumuiya ya biashara ya kimataifa.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa Tanzania France Business Roundtable iliyofanyika jijini Paris sambamba na Swahili Forum, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, alikuwa mgeni rasmi.

Kupitia makubaliano hayo, TPSF itakuwa mwanachama rasmi wa International Chamber of Commerce (ICC), hatua itakayoiunganisha sekta binafsi ya Tanzania na mtandao mkubwa zaidi wa biashara duniani.

Aidha, pande hizo mbili zimekubaliana kushirikiana katika kutangaza na kuhamasisha fursa zinazotolewa na ICC nchini Tanzania, ikiwemo huduma za biashara za kimataifa, usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, utetezi wa sera pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji.

Vilevile, makubaliano hayo yameweka msingi wa kuanzishwa kwa ICC Tanzania National Committee, ambapo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa, Tanzania inatarajiwa kuwa na ofisi rasmi ya ICC Tanzania itakayokuwa chini ya usimamizi wa TPSF.

Haya ni maendeleo muhimu yanayotarajiwa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi ya Tanzania katika biashara ya kimataifa, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushindani wa biashara za Kitanzania katika masoko ya dunia.

Hatua hii imefikiwa kufuatia juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kongamano lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambalo limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Ufaransa.

TPSF pia inapenda kutoa shukrani za dhati kwa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa kwa uratibu, ushirikiano na mchango mkubwa uliofanikisha ushiriki wa Tanzania katika shughuli hizi muhimu za kimataifa pamoja na kuwezesha kufikiwa kwa makubaliano haya ya kihistoria.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button