GEF yawa msaada wanawake kiuchumi Dar

DAR ES SALAAM; Mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa (GEF), umeleta mafanikio makubwa kuwainua wanawake kiuchumi katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo, mikopo bila riba na uanzishwaji miradi ya ujasiriamali.

Kamati kitaifa ya ushauri ya utekelezaji wa programu hiyo, iliwatembelea wanawake hao ili kujua mafanikio na changamoto zao.

Akizungumza Mbele ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa Halmashauri ya jiji, Rehema Sanga amesema jukwaa hilo kuanzia Juni 2023 hadi Julai 2024 kupitia idara ya maendeleo ya jamii dawati la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, inasimamia shughuli zote za jukwaa la kuwezesha wananwake kiuchumi kuanzia ngazi ya wilaya, kata na mitaa.

Advertisement

“Halmshauri ina jukwaa moja ngazi ya wilaya na majukwaa 36 ngazi ya kata ,mitaa 159, viongozi 288 wamepata mafunzo ya uongozi na wanawake wamekuwa wakishiriki katika matamasha na maonesho mbalimbali kama Sabasaba, Nanenae, tamasha la jua kali, tamasha la zijue fursa kataa ukatili kushiriki matamasha ya majimbo na kufanya matendo ya huruma kwa wahitaji,”amebainisha.

Amesema pia wametoa mafunzo ya uongozi na kuhamasisha uanzishawaji wa SACCOS ngazi ya kata 36, ambapo jimbo la Ukonga walioshiriki ni 84, Segerea ni 96 na Ilala ni 91.

Aidha amefafanua kuwa wanawaunganisha wanawake na fursa za mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa huduma za CRDB wanawake 343 na wamepata mikopo nafuu ,benki ya DCB wanawake 523 wamepata mafunzo ya fedha na kufungua akaunti za vikundi.

“Kwa benki ya NMB wamepata elimu wanawake 3,250 walifungua akaunti na benki za TCB wanawake 979 na pia wadau kama SIDO ,BRELA, NSSF, TRA,TBS, UTT  walitoa fursa ya mafunzo kwa wajasiriamali, leseni za biashara na fursa nyingine.

Amesema wameanzisha miradi midogodogo katika majukwaa ya kata na mitaa iliyosaidia wanawake wengi ambao hawakuwa na miradi kujishughulisha kama vile mama lishe, wauza vitafunio, kilimo cha mbogamboga ,uyoga, sabuni ambapo wanawake zaidi ya 5662 wamenufaika.

Ameeleza kuwa changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa bajeti ya usimamizi na uratibu wa majukwaa na kwa kutatua changamoto hiyo wanaomba halmashauri iwatengee fedha kwa ajili ya kuendesha shughuliza majukwaa na kuomba wadau.

Mjumbe wa Kamati hiyo Hassan Juma, ameeleza namna ambavyo majukwaa hayo ni kichocheo cha maendeleo, kwani wanawake wanapata kujikwamua kiuchumi na kuondokana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa kuwa tegemezi.

Naye mmoja wa wanufaika wa majukwaa hayo, Tatu Seif ameipongeza serikali kwa juhudi zake za kumkomboa mwanamke kiuchumi na kiuongozi kupitia majukwaa hayo, kwani fursa ni nyingi, lakini pia ameomba kuongezwa kwa maeneo ya kufanyia uzalishaji kwa wajasiriamali wa chini.