Geita wapania kumaliza uhaba vitanda vya wagonjwa

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani hapa, Paul Wanga amesema wameanza kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wanamaliza kero ya uhaba wa vitanda vya wagonjwa kwenye vituo vya afya.

Wanga amesema hayo wakati akizungumuza na waandishi wa habari, mara baada ya kukabidhi vitanda vya wagonjwa 20 katika kituo cha afya cha Kata ya Katoro, ambacho kiliripotiwa kuwa na uhaba wa vitanda.

Amesema mpango huo unalenga kuwezesha vituo vya afya kumudu idadi kubwa ya wanawake wanaofika kupata huduma, ambapo mpaka sasa kituo cha afya Katoro kinahudumia wajawazito kati ya 30 hadi 40 kwa siku.

“Hii ni sehemu tu ya vitanda ambavyo tumeagiza, jumla tumeagiza vitanda 50, kwa hiyo tumeanza na 20 hivi, ambavyo ndio vimefika tumevipokea, na kwa hiyo tunavileta hapa kituoni kwa ajili ya kuvikabidhi sasa.

“Sisi kama Halmashauri ya Wilaya ya Geita tunaendelea kukamilisha hospitali yenye hadhi ya wilaya iliyopo Katoro (mji mdogo), ianze kufanya kazi, yamkini mwezi Januari 2023 tutaanza kutoa huduma katika hospitali hiyo.

“Kwa hiyo tutapunguza msongamano mkubwa katika kituo hiki cha afya (Katoro) na wengi sasa wataenda kuhudumiwa kwenye hiyo hospitali yenye hadhi ya wilaya,” ameeleza Wanga.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Dk Modest Burchard, amebainisha vitanda 20 vya wagonjwa vimegharimu Sh milioni 14, ambapo vimeongeza idadi katika kituo cha afya Katoro kutoka vitanda 66 hadi vitanda 86.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Katoro, Dk Zakayo Sungura, amesema vitanda hivo vitaondoa tatizo la akina mama kulala wawili kwenye kitanda kimoja, baada ya kujifungua na kuwekaa mazingira rafiki ya kuwahudumia.

“Kituo chetu cha afya kimekuwa kikipata wazazi kwa mwezi wanaojifungua takribani 900 mpaka 1000 kwa miezi mitatu mfululizo, lakini hali hii huwa siyo ya kudumu kuna kipindi wanajifungua 600, 700 mpaka 800, ” ameeleza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button