Georgia Mtikila; Kinara wa demokrasia ‘asiyevuma’

‘MKE wa Mchungaji Mtikila’ ni jina linalorahisisha wengi (wafuatiliaji wa masuala ya siasa na demokrasia) kumfahamu kama si kumkumbuka. Lakini jina lake rasmi ni Georgia Mtikila.

Lakini ndugu, jamaa na marafiki walioshuhudia kuzaliwa kwake, Februari 20, 1949 na walioishi naye katika Kijiji cha Katoke, wilayani Muleba katika Mkoa wa Kagera, wanamfahamu kwa jina la Georgia Celestine.

Vivyo hivyo waliosoma naye shule ya msingi Katoke tangu mwaka 1955 hadi 1958, shule ya kati Rwamishenye 1959 hadi 1962 mkoani Kagera.

Waliosoma naye Shule ya Wasichana Bwiru mkoani Mwanza tangu 1963 hadi 1966 na wale wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa 1967 hadi 1968 pia wanafahamu jina hili kwani ndizo taasisi zilizoandika historia yake ya kitaaluma.

Aidha, ina hili liliendelea kutumika katika jshule alizofundisha mkoani Dar es Salaam kuanzia 1969 hadi 1972.  Nazo ni shule za msingi Forodhani na Tandika. Baadaye alifanya kazi katika makao makuu ya Wizara ya Elimu hadi 1982.

Aidha, waliofanya naye katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii 1982 hadi 1984 Dar es Salaam si wageni wa jina hili.

Lakini kuanzia 1984, utambulisho wa Georgia ulibadilika baada ya kuolewa na Mchungaji Christopher Mtikila. Hivyo waliofanya kazi naye katika Shule ya Kimataifa ya Dar es Salaam akiwa mhasibu 1985 hadi 1987, watakuwa wanamfahamu kwa jina la Georgia Mtikila.

Georgia aliishi na Mchungaji Mtikila hadi Oktoba 4, 2015 kifo kilipowatenganisha. Hawakujaliwa kupata mtoto katika maisha yao.

Mchungaji Mtikila alikuwa mwenyekiti wa Democratic Party (DP) na Georgia akiwa Katibu Mkuu.

“Nilikuwa mwanamke wa kwanza kuwa katibu mkuu wa chama… na nimekuwa, nadhani mwanamke wa tatu kuwa mwenyekiti wa chama ingawa sijahakikisha. Hata hivyo, naamini tuko wachache sana; wanawake wenyeviti,” anaeleza Georgia.

Anaeleza hayo katika mahojiano na HabariLEO yaliyofanyika nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam yakiangazia nafasi yake akiwa mwanamke na harakati za demokrasia na siasa kwa ujumla.

Georgia ambaye kitaaluma ni mwalimu, anatajwa kuwa kinara wa siasa aliyekuwa bega kwa bega na mumewe katika harakati za demokrasia.

Walio ndani ya DP wanasema ni vigumu kumtenganisha Georgia na harakati za siasa zilizompa sifa na umaarufu Mchungaji Mtikila.

Mwanachama na mdhamini wa DP, Anna Mkumbwa (72) anamwelezea, Georgia kuwa ni mwanamke jasiri aliyesaidia mambo mengi ndani ya chama ikiwamo kumshauri na hata kumtuliza Mchungaji Mtikila.

“Alikuwa ni backup (msaidizi) wa mume wake. Mchungaji Mtikila alikuwa na hulka ya uamuzi wa haraka. Akitaka kuamua kitu akiwa na uhakika na kitu, hakuwa na shida ya kufikiri mara mbili, alikifanyia kazi haraka na kwa kasi kiasi ambacho Georgia ilibidi aingilie kati. Akisema hapo hapana, na mumewe alimsikiliza,” anasema Anna.

Kutokana na uwezo wa Georgia, Mtikila alipokutwa na mauti Oktoba 4, 2015 kutokana na ajali ya gari katika Kijiji cha Msolwa karibu na Chalinze, mwanamke huyu alichaguliwa na wanachama Mei 26, 2017 kuongoza DP.

Hata hivyo, mwezi uliofuata palitokea mabadiliko ya uongozi ambayo Georgia hapendi kuyazungumzia kwa undani kwa kile anachosema suala hilo liko mikononi mwa mamlaka za serikali kwa ajili ya kupata suluhisho. “Nisingependa kulizungumzia kwa sababu kuna mamlaka zinalishughulikia,” anasema.

Mwenyekiti wa DP Mkoa wa Shinyanga na mshauri kutoka taasisi ya Liberty International Foundation, Mohamed Simba anadokeza mabadiliko hayo akisema yamemrudisha nyuma Georgia katika harakati za siasa.

“Juhudi za mama Mtikila katika siasa ni kubwa, lakini baada ya mchungaji Mtikila kufariki na mama kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama, msajili (wa vyama vya siasa) hakumtambua,” anasema Simba.

Simba anasema chama kimevamiwa na watu ambao wanadai ni viongozi, hali ambayo imerudisha nyuma harakati za Georgia katika siasa kwani watu hao wametambuliwa na ofisi ya msajili.

“Huyu mama ni mtetezi mzuri… hata katika harakati za Mchungaji Mtikila, alikuwa ni injini, ndiye alikuwa mwanamipango katika DP. Marehemu (Mtikila) alikuwa mwanasheria na alikuwa na purukushani nyingi.

“Lakini mpanga mipango na kuonesha dira ya chama alikuwa ni mama Mtikila, ndiyo maana tulimchagua sisi kuwa mwenyekiti wetu lakini sasa kitu kinachonisikitisha, msajili hakumtambua na mpaka sasa hajamtambua, chama kimevamiwa na watu ambao si wana demokrasia,” anasema Simba.

Mwanachama mwingine wa DP, Gervas Mwesiga anasema, “Unapozungumzia harakati, umaarufu na nafasi ya mchungaji Mtikila katika siasa na demokrasia, sisi tuliokuwa ndani ya chama tunafahamu wazi kwamba ni vigumu kumuengua, Georgia. Huyu mama alikuwa sambamba naye… umma unaweza usifahamu hilo.”

“Mama Mtikila hajabahatika kupata nafasi ya kujulikana kama ya akina mama Mongela (Getrude) na wengine ambao ni maarufu, lakini waliyofanya (na Mtikila) kwenye demokrasia ni makubwa.”

Anamwelezea Georgia kwamba alikuwa sambamba na Mtikila kwenye harakati za haki za binadamu na siasa tangu wakiendesha Shirika la Liberty International Foundation kabla ya DP.

Aeleza siri kuingia siasa

Katika mahojiano, Georgia analithibitishia HabariLEO hayo yanayosemwa kumhusu katika harakati za siasa na demokrasia na kueleza kilichomsukuma kuungana na mumewe.

“Niliingia kwenye siasa kwa ajili ya kumsaidia Mchungaji Mtikila. Lakini yeye ndiye mentor (mfundaji) wangu wa siasa. Baada ya kuingia na kuangalia akaniongoza nikawa kama hivi nilivyo,” anasema.

Georgia ana mengi ya kumwelezea Mtikila alivyomlea si tu kisiasa bali pia kijamii akisema, “Halafu alikuwa baba yangu, mume wangu na alilea familia vizuri.”

 

Georgia akiwa na Mchungaji Mtikila.

“Yaani mimi nilikuwa sijui kitu chochote… analeta nguo, analeta kila kitu mpaka na mafuta… Sasa baada ya kuondoka (kufariki), kuna wanawake walikuwa wananiletea vitu wanasema tunajua hata sokoni ulikuwa hujui. Kwa hiyo, nilikuwa nawaomba hawa vijana wangu nawaeleza, msije mkanilea kama Mchungaji Mtikila alivyonilea. Alikuwa ni baba mzuri aliyejali familia,” anasema na kuongeza kwamba hata wangekosa fedha, ndani ya nyumba hapakukosekana chakula ambacho Mtikila alihakikisha kinakuwapo.

Alivyojitosa kwenye siasa

Akieleza historia yake ya harakati za siasa na demorasia, Georgia anasema alianzia harakati za kutetea binadamu kupitia Liberty International Foundation.

“Wakati huo, demokrasia ilikuwa inaongelewa kwa mbali na siasa ilikuwa ya chama kimoja na ilikuwa ya watu fulani hivi,” anasema Georgia.

Anasema 1986, mchungaji Mtikila alianza kuzungumzia juu ya kutetea Tanganyika na mambo yanayoendana na haki za nchi.

“Hili lilinitia hofu sana kwa sababu ilisababisha kukamatwa kwake mara kwa mara. Niliona ili kumaliza au kupunguza hofu hii, niungane naye, nijue angalau anafanya nini na yuko wapi wakati akiwa hayupo nyumbani,” anasema Georgia.

Anasema aliingia moja kwa moja katika harakati za demokrasia chini ya mfumo wa vyama vingi 1992 katika kipindi ambacho Mtikila alikumbwa na misukosuko mingi.

“Kilichonisukuma kuingia kwenye siasa, kwanza ni kwa ajili ya Mchungaji jinsi alivyoanza na kukamatwa kwake. Nikaona huyu mtu nisipomfuatilia, inaweza ikawa tatizo. Ndipo nikaanza kufuatilia. Saa nyingine barua zake za kuisema serikali zinakuwa kali, anatumia maneno makali ya kuwasahihisha wanakasirika wanakuja kumkamata,” anasema Georgia.

“Sasa mimi mambo ya kukamatwa kamatwa sikuyapenda. Kwa hiyo nikawa nafuatilia hizo barua namwambia nitazipeleka mwenyewe. Nikiona barua inaleta utata, naificha. Ananiuliza imefika, nasema imefika,” anaeleza.

Georgia akiwa na mwandishi wa makala haya.

“Na alipogundua kwamba ninazificha (baadhi ya barua), akawaweka vijana na vijana tukawaomba, jamani huyu baba atakamatwa mpaka lini? Kwa hiyo tukawa barua nyingine tunazizuia lakini akaja kugundua.” Hata hivyo anafafanua kwamba hilo alilifanya kwa nia njema ya kumlinda ili ‘kamata kamata’ isiwe chanzo cha kumvunja nguvu kupambania demokrasia.

Anasema baada ya kuingia kwenye siasa, alizoea na kumudu. “Nikaanza kwenda kwenye mikutano, mara ananituma nakwenda mwenyewe, ndipo nikaja kuwa kiongozi. Sasa namudu na naweza kujiongoza mwenyewe siyo kichwa chake.”

Vikwazo kisiasa

Hata hivyo anasema alipoingia kwenye siasa pamoja na Mtikila, baadhi ya watu wa karibu naye walionesha kutopendezwa na uamuzi wao wa kuingia kwenye vyama vya siasa wakiwaambia kwamba ni kutafuta usumbufu usio wa lazima.

“Kusema kweli, neno la Mungu lilinisaidia na hata sasa linanisaidia sana. Nikisikia mtu anasema kitu juu yangu, kama si kosa, huwa sijali. Na tabia hii inanisaidia katika mambo mengi,” anasema.

Anasema alisimamia dhamira yake ya kutetea maendeleo, ustawi wa nchi na watu wake, hivyo hakuona kama ni kosa la kumfanya awasikilize waliokuwa wakiwabeza.

Georgia anajivunia kwa kuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza walioanzisha vyama vya siasa kisha kushika nafasi ya juu, akisema ni alama isiyofutika katika maisha yake.

Georgia na ‘Siasa za kukamatwa’ 

Georgia anasimulia alivyobeba mzigo pale, Mchungaji Mtikila alipokamatwa, ikiwa ni pamoja na kwenda kumuona akiwa mahabusu/gerezani. Anasema aliwajibika kwanza kama kiongozi wa DP na pia, akiwa ni mke.

Anakumbuka Mtikila alipofungwa mwaka mmoja 1999 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno kumhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba (marehemu).

Anasema yeye na viongozi wa DP walipofika gerezani, alishindwa kujizuia kwa kumuona mwenyekiti na mumewe akiwa amechuchumaa mbele yao.

“Nilipiga magoti na kulia nikamwambia askari, huyu ni mwenyekiti wetu na mume wangu tunamheshimu, iweje achuchumae mbele yetu?” anasema baadaye askari walimruhusu akasimama na kuongea nao.

Anakumbuka siku nyingine Mtikila alipokuwa mahabusu ambayo alikwenda kumuona lakini akakataliwa akiambiwa kuna watu wengine wameshakwenda. “Niliangua kilio, nilipiga ukunga nikisema…Iweje nikataliwe kumuona?’’

Hata hivyo, Georgia anasema alikuwa akimsihi Mtikila ‘kulegeza’ harakati zilizochangia akamatwe akimweleza kuwa wakati mwingine zinaathiri upatikanaji haraka wa kile wanachodai.

“Kuna wakati nilimwambia kuwa kama hutaacha siasa za kufungwa sitakuja Keko (gereza),” anasema Georgia ingawa anasisitiza kuwa halaumu kwa kuwa ndiyo njia aliyoichagua kati ya njia nyingi za kudai haki.

“Nyote mnaweza kuwa na nia ya kufika mahali. Kila mtu akatumia njia yake. Lakini njia nyingine inaweza kukuchelewesha kufika ingawa nyote mnaweza kufika.”

Georgia anafafanua kwamba ‘siasa za kukamatwa’ wakati mwingine huchelewesha haki, akirejelea DP ilivyochelewa kupata usajili wa kudumu kutokana na mchungaji kukataa kuitambua Zanzibar.

Anaeleza tofauti kati ya siasa za ‘nguvu’ na za ‘maridhiano’ akirejea msemo (wa kabila lake) akiutafsiri, ‘Kwa shujaa wanalia, kwa mwoga wanacheka’.

Awausia wanawake

Anashauri wanawake kuunga mkono wenza wao katika siasa vivyo hivyo kwa wanaume akisisitiza kwamba siasa ni kitu chema. “Siasa ni kitu cha Mungu, siasa ni kuwasaidia watu ili tuenende mwendo mzuri. Wanaoharibu ni watu, si siasa yenyewe.”

“Nawaomba wanawake waingie kwenye siasa na wafanye siasa zilizo njema za kuwasaidia wananchi… Tusibweteke, tupambane.”

Anasema wanawake wanaweza kusimama wenyewe na kuleta tija. “Si mnaona tuna Mama Samia sasa ni Rais (Suluhu Hassan)…”

Anamsifu kwa ubunifu ikiwamo kuitangaza nchi kimataifa kupitia utalii, akisema amewaheshimisha wanawake.

“Kulikuwa na dhana kwamba mwanamke hawezi kuongoza nchi. Lakini Mama Samia amedhihirisha kuwa wanawake tunaweza,” anasema.

Anafafanua, “mimi ni chama cha upinzani, lakini pale mtu au kiongozi anapofanya vizuri ni vizuri kueleza na anapofanya isivyo, pia tunaeleza.”

Anahadharisha wanawake kutobweteka kwa kuwapo rais mwanamke. Anawahimiza waungane kung’oa mizizi ya mtazamo hasi dhidi ya mwanamke.

Anataja mizizi hiyo ni utamaduni na wa imani inayoaminisha kwamba mwanamke hafai kuwa kiongozi wa kisiasa. “Ni lazima tuungane bila kujali itikadi za kisiasa kuhakikisha mwanamke anasonga mbele”.

Anashukuru Jukwaa la Wanawahabari Wanawake (WRIFOM) chini ya mradi wao wa wanawake na demokrasia unaoibua na kutambua wanawake (akiwamo) wenye mchango mkubwa katika siasa na demokrasia nchini.

Mradi huo unatekelezwa kupitia wanahabari wanawake (akiwamo mwandishi wa makala haya) ambao wanafanya mahojiano ya kina kuhusu wanawake wenye mchango mkubwa katika demokrasia na kuchapisha habari zao.

“Nawashukuru ninyi (HabariLEO) kwa kuona nastahili kuandikwa… ni kweli nilikuwa sambamba na Mchungaji Mtikila na najua utamu na uchungu wa kupambania demokrasia,” anasema Georgia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button