GGML yaungana na Takukuru kukabili mianya ya rushwa

GEITA: KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu ya Geita (GGML) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) imekuja na kampeni ya utoaji elimu kwa jamii kukabiliana na tatizo la rushwa.

Kampeni hiyo ilianza na warsha ya siku mbili kwa wadau wa maendeleo, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa na wakandarasi wote wanaohusika na mnyororo mzima wa thamani katika shughuli za GGML.

Ofisa Mahusiano Mwandamizi wa GGML, Gilbert Mworia amesema hayo Mei 14, 2025 baada ya kuhitimishwa kwa warsha hiyo iliyofanyika mjini Geita na kusisitiza kuwa lengo ni kuongeza uwazi hususani katika ajira na manunuzi.

Amesema, GGML kwa mwaka inafanya manunuzi ya zaidi ya Dola milioni 300 ambayo iwapo hayatafuata miongozo ya nchi na taratibu za kampuni huenda yakaiweka kampuni katika wimbi kubwa la rushwa.

Mworia amesema kwa kutambua hilo ndio maana GGML na Takukuru wamejidhatiti kuongeza uelewa wa jamii katika kukemea, kupinga na kuzuia viashiria na vitendo vyote vya rushwa.

Mworia amesema kwa kutambua hilo ndio maana GGML na Takukuru wamejidhatiti kuongeza uelewa wa jamii katika kukemea, kupinga na kuzuia viashiria na vitendo vyote vya rushwa.

“Tumeelezea jinsi gani tunafanya manunuzi, jinsi gani tunaajiri watu, jinsi gani tunatekeleza miradi yetu ya CSR, jinsi gani kama kuna viashiria vya rushwa tunaweza kupewa taarifa.

“Kampuni yetu sasa hivi imesajiliwa kwenye NewYork Stock Exchange, kwa hiyo bila kufuata kanuni, taratibu na sheria mbalimbali basi tunaweza tukaamuka tukashangaa mgodi umefilisika”, amesema.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombat amesema warsha imetoa fursa ya kujadiliana na kuweka mikakati ya pamoja ili kuzuia rushwa katika shuguli za manunuzi na utekelezaji wa miradi.

Amesema iwapo huduma za mgodi zitatolewa kwa kuzingatia taratibu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyopo katika sekta ya madini adhima ya uwezeshaji wazawa itafanikiwa kwa vitendo.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge amesema rushwa inaathiri mapato ya serikali, kuvuruga ushindani wa haki katika masoko na inapunguza imani ya wanachi kwa mfumo wa utawala.

Meneja Mahusiano, Ako Group Ltd, Waisile Baire amekiri kuwa mianya ya rushwa imekuwa kikwazo kikubwa katika mnyororo wa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi hivo hatua zikichukuliwa itachagiza mabadiliko chanya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button